Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

Mradi wa Uboreshaji wa Reli ya kati(TIRP)

Mradi wa ukarabati wa njia ya reli ya kati ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia unajulikana kama ‘Tanzania Intermodal and Rail Development Project’ (TIRP). Mradi huu unagharimu pesa za Kimarekani Dola Milioni 300.

Madhumuni ya Mradi

Kuwa na usafiri wa Treni unaoaminika kutoka Dar es salaam hadi Isaka.

Taarifa za Mradi

Mradi umelenga kufanya ukarabati wa Reli iliyopo kwa kipande cha Dar es salaam-Isaka (km 970) ili kuongeza uwezo wa kubeba mzigo toka chini ya Tani 13.5 za uzito wa ekseli hadi tani 18.5 kwa kufanya yafuatayo;

  • Kutandika upya njia za Reli zenye uzani wa paundi 80 kwa umbali wa Kilometa 312.
  • Kufanya ukarabati wa njia ya Reli kwa urefu wa Kilometa 658.
  • Kufanyia ukarabati wa makaravati na madaraja 442.
  • Kuboresha mfumo wa mawasiliano.
  • Ukarabati wa vituo vya kupakia na kupakua mizigo vya bandari ya Dar es salaam, Ilala na Bandari kavu ya Isaka.
  • Zaidi ya ukarabati wa njia, kupitia mradi huu tutaweza kununua mitambo ya ukarabati wa njia, vichwa vitatu vya treni(vipya) na mabehewa mapya 44 ya mizigo, na kukarabati vichwa viwili vya treni.

Faida za Mradi

Faida za Mradi wakati wa Ujenzi

  • Kuwepo kwa fursa za ajira.
  • Kukua kwa kipato cha wananchi maeneo ya mradi.
  • Kujengewa ujuzi kwa wote watakaoshiriki kwenye shughuli za ujenzi.

Faida za mradi baada ya kukamilika

  • Kuboresha na kuongeza kiwango cha ubebaji mizigo kwa miundombinu ya reli na madaraja.
  • Kuongezeka kwa mwendokasi wa treni toka Kilometa 30 kwa Saa hadi kufika Kilometa 70 kwa Saa na hivyo kupunguza gharama za usafirishaji.
  • Kupunguza muda wa kupakia na kupakua mizigo kutoka Bandari ya Dar es salaam hadi bandari kavu ya Isaka kufikia Saa 24.
  • Kutengenezwa kwa mpango endelevu wa matengenezo ya miundombinu ili kufanya usafiri huu kuwa wa uhakika na kuaminika.
  • Kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Reli na hivyo kuongeza ufanisi katika kutoa huduma.
  • Kupunguza gharama za matengezo ya barabara na hivyo serikali kuelekeza bajeti iliyookolewa kwenda huduma nyingine ya kijamii.

Maendeleo ya Mradi

  • Mradi huu ni ukarabati wa reli iliyopo ya kiwango cha kawaida (Meter Gauge Railways).
  • Mradi huu umegawanyika katika vipande viwili, kipande cha kwanza kitaanzia Dar es salaam hadi Kilosa (Kilometa 283) na Kipande cha pili ni Kilosa hadi Isaka (kilometa 687).
  • Vipande hivi vimeshapata wakandarasi na ujenzi unatarajiwa kuanza mapema Juni 2018.
  • Kwa sasa hatua mbalimbali za matayarisho ya ujenzi zinaendelea.

Mambo ya Kuzingatia wakati wa Mradi

  • Hairuhusiwi kufanya biashara yoyote katika maeneo ya stesheni bila kibali maalumu.
  • Vibali vya biashara vinapatikana katika kila stesheni bure, hivyo mfanyabiashara unapaswa kujiandikisha kupata kibali chako.
  • Wafugaji wote hawaruhusiwi kabisa kufanya shughuli za ufugaji katika maeneo ya mradi hivyo watapaswa kuendesha shughuli hizo mbali na eneo la ujenzi.
  • Wakulima wote wanaofanya shughuli za kilimo katika eneo la mradi watapaswa kusitisha kabisa shughuli za kilimo katika maendeleo ya reli ifikapo mwisho wa mwezi Mei 2018.
  • Tahadhari za kiafya ni muhimu kuzingatiwa kwa wananchi wote kwa kuepuka ngono zembe kwani kutapelekea ongezeko la maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama vile ukimwi, kaswende pamoja na mimba zisizotarajiwa.
  • Vitendo vyovyote vya kikatili vinapaswa kutolewa taarifa mara moja katika ofisi husika za serikali na pia kupitia anuani na namba zetu za simu.
  • Epuka kukaa, kuvuka na kuzurura katika maeneo ya reli kwani kunaweza kupelekea kujeruhiwa au kifo.
  • Wananchi wote mnashauriwa kuchangamkia fursa mbalimbali za ajira na biashara zinazotokana na mradi huu.