Maelezo ya Jumla
Utangulizi
Shirika la Reli Tanzania, ni shirika lililoundwa chini ya Sheria ya Reli Namba 10 ya mwaka 2017 kwa lengo kuu la kutoa huduma ya usafiri bora na uhakika wa reli, Kusimamia, kuendeleza na kuhakikisha ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli nchini Tanzania.
Historia
Historia ya Shirika la Reli Tanzania inaweza kuanza kutajwa mnamo mwaka 1948 lilipoanzishwa Shirika la Reli na Bandari za Afrika Mashariki (EAR&H). Shirika la reli na bandari za Afrika ya Mashariki liliundwa mnamo mwaka 1948 sambamba na Jumuiya ya Afrika Mashariki na lilikuwa Shirika la umma lililosimamia reli na bandari za Kenya, Uganda na Tanganyika na baadaye Tanzania katika miaka kabla na baada ya uhuru wa nchi hizi.
Baada ya kuvunjika kwa jumuiya ya Africa Mashariki, Shirika jipya la Reli (Tanzania Railways Corporation) liliundwa kama Shirika la Umma. Shirika la Reli Tanzania liliendelea kubeba jukumu zima la usafirishaji nchini Tanzania hivyo kuendelea kutoa huduma za usafiri kwa njia ya reli (Reli Transport Services), majini (Marine transport service), Barabara (Road transport service) na huduma za Mahoteli na Migahawa (Hotels and Catering services). Shughuli za usafirishaji nchini Tanzania ziliendelea kwa kutumia nyenzo zilizokuwepo, kwa sababu vifaa vingi vilizuiliwa Nairobi –Kenya, ambako ndiyo yalikuwa makao makuu ya Jumuiya na pia makao makuu ya Shirika la Reli la Afrika Mashariki.
Ubinafsishaji wa Shirika la Reli Tanzania
Kutokana na ukweli kuwa, juhudi za kulifanya Shirika lijiendeshe kwa faida hasa baada ya mipango ya ERP na RRP kutofikia viwango vilivyotarajiwa mwishoni mwa miaka ya 1990 wafadhili waliamua kusitisha kuendelea kuwekeza katika usafiri wa reli na wakasisitiza sera ya ubinafsishaji.
Malengo ya Kubinafsisha usafiri wa Reli yalikuwa,
- Kushirikisha wawekezaji kutoka sekta binafsi
- Kushirikisha menejimenti kutoka sekta binafsi
- Kuipunguza serikali mzigo wa shirika kutegemea bajeti ya serikali
- Kuingiza teknolojia za kisasa katika utendaji
Mnamo mwaka 1998 Serikali iliidhinisha mpango wa ubinafsishaji wa Shirika la Reli Tanzania uliotarajiwa kuanza April, 1998 na kumalizika Aprili 2000. Baada ya mchakato mrefu, tarehe 6 Machi 2006 kampuni ya RITES ya India ilipewa taarifa ya ushindi na baada ya taratibu zote kutimizwa ikiwemo kuanzishwa kwa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), uongoozi wa RITES ulikabidhiwa uendeshaji wa huduma za usafiri wa Reli ya Tanzania kwa kipindi cha miaka Ishirini na tano kuanzia Octoba 1, 2007. RITES ya India ilikuwa na 51% ya hisa zote na Serikali ya Tanzania ilikuwa na 49%.
Hata hivyo malengo yaliyotarajiwa kupatikana baada ya ubinafsishaji yalidhihirika kutofikiwa, Serikali ya Tanzania iliamua kusitisha mkataba wa ukodishwaji mnamo mwaka 2010 na kuanzia tarehe 22 Julai 2011 kampuni ilirudi mikononi mwa serikali kwa umiliki wa asilimia mia moja(100%).
Kuundwa upya kwa Shirika la Reli Tanzania(TRC)
Mnamo mwaka 2017 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha muswada wa Sheria ya Reli Tanzania ili kuziunganisha Kampuni ya Reli Tanzania(TRL) na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli(RAHCO) na hatimaye kuundwa kwa Shirika la Reli Tanzania(TRC) chini ya Sheria mpya ya Reli Tanzania.