ZOEZI LA UTWAAJI ARDHI KUPISHA UJENZI WA SGR MKOANI TABORA LAENDELEA

March
2023
Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na utekelezaji wa utwaaji ardhi kwa matumizi ya ujenzi wa reli ya kisasa – SGR mkoani Tabora katika kipande cha tatu (3) Makutupora – Tabora ambapo ujenzi umefikia 5.52%, Machi 09, 2023.
Timu ya maafisa kutoka TRC ilianza kwa kufanya uhamasishaji kwa viongozi wa Serikali kwa ngazi ya wilaya, vijiji na kata pamoja na wananchi ambao ni walengwa katika zoezi, uhamasishaji umefanyika ukiwa na lengo la kuwaelimisha wananchi na viongozi kuhusu utaratibu na namna zoezi la kuhamisha makaburi litakavyoendeshwa kwa kuzingatia Sheria ya ardhi na kanuni za afya.
Mara baada ya uhamasishaji zoezi la kuhamisha makaburi lilianza rasmi katika kijiji cha Itulu, kata ya Ndevelwa Manispa ya Tabora ambapo jumla ya makaburi 74 yamehamishiwa katika sehemu nyingine iliyotengwa na Serikali za vijiji kwa lengo la kupisha ujenzi wa reli ya kisasa.
Katika hatua nyingine, viongozi wa mkoa wametoa wito kwa Serikali ya kijiji na ndugu wa marehemu kutoa ushirikano wa kutosha ili kuhakikisha zoezi linaenda salama na hatimaye kukamilika na mkandarasi kuendelea na ujenzi wa reli ya kisasa.
Sambamba na hivyo zoezi limesimamiwa na kuratibiwa na viongozi mbalimbali na wataalamu wa afya, wahandisi, maafisa ardhi, maafisa jamii, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa vijiji, kata, tarafa pamoja na viongozi wa Dini, hata hivyo zoezi la uhamishaji makaburi ni endelevu kwa sasa limeanza kufanyika katika manispaa ya Tabora katika kijiji cha Itulu na badaye mkoani Singida katika wilaya ya Manyoni.