KARAKANA YA TRC MOROGORO YAFUFUA VICHWA VITANO VYA MGR
June
2026
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Masanja Kungu Kadogosa, Juni 13, 2026 imefanya ziara katika karakana ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) ya matengenezo, ufufuaji na uboreshaji wa vichwa vya treni Mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Mhe. Kadogosa amesema kuwa lengo la ziara hii ni kukagua maendeleo ya ukarabati, ufufuaji na maboresho ya vichwa vya treni ambapo mpaka sasa Shirika limefanikiwa kufufua vichwa vitano na hatua hii imewezesha kuongeza uzalishaji wa Shirika.
"Karakana ndo moyo wa reli na kazi hii ya ukarabati na ufufuaji inahitaji pesa na sisi Kamati PIC tutahakikisha taasisi zilizotengewa mfuko maalumu zipate hizi pesa kwaajili ya kuendeleza kazi kama hii ya Karakana, tunaipongeza sana Wizara ya Uchukuzi na Shirika la Reli kwa ubunifu huu, ameongeza Mhe. Kadogosa.
Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa Serikali imepunguza gharama za kuagiza vichwa vya treni za MGR nchini Malyasia kwa kuimarisha upatikanaji wa vifaa na kufanya matengenezo ndani ya nchi kupitia TRC Karakarana ya Morogoro.
Karakana ya Morogoro yenye jumla ya watumishi 121 kwa sasa inahudumia jumla ya vichwa vya treni 68 vinavyojumuisha vichwa vya njia kuu 50 na vya sogeza 18 na pia inaendelea kusimamia matengenezo yaliyopangwa na ya dharura.

