Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​ZOEZI LA FIDIA LAENDELEA MKOANI TABORA


news title here
22
May
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliotwaliwa maeneo kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha tatu Makutupora - Tabora lililoanza katika mtaa wa Itulu katika kata ya Ndevelwa wilaya ya Tabora Manispaa mkoani Tabora Mei, 2023.

Afisa Ardhi kutoka TRC Bw. Sweetbert Misango alisema kuwa zoezi hilo ni kwaajili ya wananchi ambao maeneo yao yamepitiwa na njia kuu ya reli ya kisasa katika mradi wa ujenzi wa SGR.

“Maeneo mengi ambayo yametwaliwa na mengine yameshafanyiwa uthamini hivyo malipo haya ni kwaajili ya njia kuu, kwa maeneo mengine bado mchakato wa malipo unaendelea ili wananchi wote wakabidhiwe stahiki zao” alisema Bw. Misango.

Mtendaji wa serikali ya mtaa ya Itulu Bw. Bariki Kaponda ameeleza kuwa wananchi wamekua wakisubiri malipo hayo kwa hamu ili kupisha ujenzi ambao utaleta manufaa katika mkoa wa Tabora na nchi kwa ujumla.

“Mradi huu ni wetu sote na serikali inafanya vyema kulipa fidia na kufanya wananchi wake wanahamia maeneo mengine kwa amani” alisema Bw. Kaponda.

Naye Mwananchi kutoka katika mtaa wa Itulu mkoani Tabora ndugu Mohamedi Pandauyaga alishukuru sana serikali kupitia TRC kwa kuendeleza uhusiano mzuri kwa wananchi katika maeneo yote yaliyotwaliwa na kuzidi kutoa elimu juu ya kuwekeza katika maswala ya maendeleo na kujenga makazi mazuri kwa kufuata mipango miji katika maeneo mapya.

Kipande cha tatu cha mradi wa ujenzi wa SGR Makutupora Tabora chenye jumla ya kilometa 368 hadi sasa kimefikia asilimia 7.57 ambapo ujenzi bado unaendelea katika maeneo mbalimbali yakiwemo eneo la kambi pamoja na njia kuu ya reli ya kisasa.