Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAENDELEA YA ZOEZI LA UTWAAJI ARDHI MRADI WA SGR TABORA - KIGOMA


news title here
23
December
2025

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la utwaaji ardhi kupisha mradi wa ujenzi wa reli yenye kiwango cha kimataifa - SGR kipande cha sita Tabora - Kigoma linalofanyika katika wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Zoezi hilo ni kwaajili ya kupisha ujenzi wa njia kuu ya mradi wa SGR ambapo zoezi hilo la utwaaji ardhi linahusisha uhamishaji makaburi katika vijiji sita vikiwemo kijiji cha Nyangabo, Chakulu, Bweru, Malagarasi, Nguruka na Mpeta.

Mhandisi mradi kutoka TRC Bw. Benedict Mashimbi alieleza kuwa zoezi hilo litafanyika kutoka kipande cha kuanzia kilometa 195 mpaka kilometa 250 za kipande cha Tabora - Kigoma.

Aidha Mhandisi Mashimbi alisema kuwa zoezi hilo linazingatia taratibu na miongozo ambapo timu kutoka TRC imeshirikisha ngazi mbalimbali za uongozi ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa mkoa, Mkuu wa wilaya, ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Uvinza, maafisa afya, viongozi wa dini pamoja na viongozi wa vijiji.

“Tulihakikisha tunaongea na wananchi hususan wahusika ili waweze kupata uelewa, taratibu na miongozo kwa lengo la kufanikisha zoezi bila mkanganyiko wa aina yeyote” alieleza Mhandisi Mashimbi.

Naye Afisa Afya mazingira kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Bw. Hussein Katelanya alieleza kuwa zoezi linafanyika kitaalamu ili kuzuia maambukizi na milipuko ya magonjwa kwa kuwa na vifaa kinga vikiwemo madawa,barakoa,vikinga mikono, ovaroli na mabuti.

“Kazi yetu kubwa ni kusimamia viwango vya ubora na usalama na kufuata taratibu zote zinazohusu maziko ya staha na kinga ya maambukizi pamoja na kuzuia milipuko ya magonjwa” alisema Bw. Katelanya.

Naye kaimu afisa mtendaji kutoka kijiji cha Mpeta Bw. Jelas Balegele ameeleza matarajio wa wananchi katika kupata ajira kwenye mradi wa SGR kupitia uongozi wa vijiji.

Wananchi wanaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika zoezi la utwaaji ardhi kupisha ujenzi wa SGR katika kipande hicho cha Tabora - Kigoma.