ZAIDI YA KATA 15 ZAPEWA ELIMU YA UELEWA KUHUSU USALAMA NA ULINZI WA MIUNDOMBINU YA RELI YA KISASA - SGR

August
2021
Shirika la Reli Tanzania - TRC limeendelea na kampeni ya uelewa kwa jamii kuhusu usalama na ulinzi wa miundombinu ya Reli ya kisasa – SGR katika awamu ya kwanza ya mradi Dar es Salaam mpaka hadi Morogoro, ambapo Shirika limefanikiwa kuzifikia zaidi ya Kata 15 katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, Agosti 2021.
Aidha, elimu hii ni endelevu kwa jamii ambayo inaishi maeneo yaliyo karibu karibu na mradi wa SGR unaoendelea kutekelezwa. Shirika limekuwa likitoa elimu mtambuka katika jamii hizo kwa lengo la kuwapa uelewa wananchi kuhusu mambo ambayo jamii inapaswa kuelewa ili kuepukana na changamoto mbalimbali wakati wa ujenzi na hata baada ya ujenzi kukamilika.
Hivi karibuni Shirika la Reli nchini kupitia kitengo cha usalama na ulinzi wa reli TRC lilianza kampeni maalumu ya kutoa elimu ya usalama na ulinzi wa miundombinu ya reli ya kisasa - SGR, Kampeni hiyo imeanza kutokana na mradi huu kuwa ukingoni kumalizika, hivyo umuhimu wa kutoa elimu mapema ni mkubwa ili kuzifanya jamii zilizo pembezoni mwa mradi kuwa salama na kuhakikisha ulinzi wa mradi.
Katika hatua nyingine, kitengo cha ulinzi na usalama wa reli kwa kushirikiana na kitengo cha Jamii TRC wameendelea kutoa elimu katika ushirikishwaji wa jamii kuhusu ulinzi na utunzaji wa miundombinu ya reli na kuwataka wananchi kulinda miundombinu hiyo ili kuepusha madhara yatokanayo na uharibifu ikiwemo wizi wa miundombinu na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa Shirika la Reli au vyombo vya Serikali.
Shirika limewataka wananchi kuzingatia matumizi ya alama za usalama wa reli kwenye maeneo ya vivuko, hifadhi ya reli, na maeneo ya miradi ambapo wameombwa kupita kwa tahadhari kwa kufuata alama elekezi pamoja kutojihusisha na vitendo vya uhujumu miundombinu ya reli ikiwemo kuweka vitu hatarishi kwenye reli.
Naye Mhandisi Fredirick Kitaly kutoka kitengo cha ulinzi na usalama wa reli alitoa elimu kwa walimu, wanafunzi na wazazi wa wanafunzi wa shule za misingi zilizo katika maeneo ya karibu na miundombinu ya reli kwa kuwataka wazazi na walimu kuwa mabalozi wazuri kwa kuwaelimisha watoto kuhusu miundombinu ya umeme na athari zake pale watakaposhindwa kuzingatia alama zilizowekwa.
“Ndugu zangu wazazi reli hii ya kisasa itaendeshwa kwa miundombinu ya umeme ambao ni mkali, kuna nguzo ambazo zimebeba nyaya za umeme, ninawaomba muwaambie watoto wasichezee nguzo hizo wala kukwea, kuna maeneo ambayo kuna vituo vya kupozea umeme, maeneo hayo ni hatari watoto wasicheze maeneo hayo, nawaomba elimu hii iwafikie watoto na mzidi kuwakumbusha mara kwa mara” alisema Mhandisi Kitaly.
Kwa upande wake Afisa Jamii TRC, Tumaini Rikanga alijikita zaidi katika kuwaelimisha wananchi kuhusu wajibu wa Shirika kumlinda mwananchi dhidi ya athari za mradi na mwananchi kuwajibika katika kulinda na kutunza miundombinu ya reli, hata hivyo alisisitiza jamii kutoa taarifa kuhusu vitendo vyovyote vya kikatili watakavyofanyiwa wananchi waishio maeneo ya mradi.
“Ningependa kuweka mkazo kwa wananchi wote vitendo vya uhujumu miundombinu ya reli vinaweza kuhatarisha usalama wa reli na wananchi, hivyo ni wajibu wenu kulinda reli yetu. Kila mwananchi analo jukumu la kuhakikisha miundombinu ya reli inalindwa na inakuwa salama muda wote” alisema Bi. Tumaini.
Maafisa kutoka TRC wametoa wito kwa wananchi wote na jamii kwa ujumla kwamba ni muhimu wote kwa ujumla kuwa walinzi wa miundombinu ya reli ya kisasa kwani mradi huu umetumia gharama kubwa katika ujenzi ambazo ni fedha za watanzania wao wenyewe, pia wamewataka wananchi kutoa taarifa kwa shirika na Serikali za mitaa dhidi ya vitendo vya uhujumu miundombinu ya reli.