TRC YAUNGANA NA RAIS SAMIA UPANDAJI WA MITI JAN. 27
January
2026
Shirika la Reli Tanzania (TRC) likishirikiana na wadau mbalimbali, limepanda jumla ya miti 150 katika stesheni ya abiria ya SGR na stesheni ya mizigo Januari 27, 2026.
Zoezi hilo la upandaji miti ni muendelezo wa kuungamkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kupanda miti kila ifikapo Januari 27, kama sehemu ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa.
Katika Stesheni kuu ya Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma, zoezi hilo liliongozwa na Afisa utumishi Mkuu Bw. Cornel Kyai, ambae ameeleza kuwa miti zaidi ya 150 imepandwa katika stesheni hiyo Pamoja na Kituo cha kupakia na kupakua mizigo cha treni za kisasa, Ihumwa jijini humo.
“Hili ni jambo jema kwasababu linatuhusu sote nani jambo endelevu, hautunzi mazingira kwaajili yako wewe bali kwaajili ya vizazi vijavyo” alisema Kyai.
Ameongeza kuwa zoezi hilo pia limefanyika katika mikoa mingine iliyopitiwa na reli ikiwemo Morogoro na Dar Es salaam.
Katika hatua nyingine, taasisi za Uchumi na Maendeleo za Organization (UMO) na Dodoma City Legends Family (DCLF) pia zimeshirikiana na TRC katika zoezi hilo huku vijana wakiwa sehemu kubwa ya washiriki.
“kushiriki katika zoezi hili ni muhimu lakini vilevile tutakwenda kutoa elimu kwa jamii ya hapa Dodoma kuhusu utunzaji wa mazingira, hasa upandaji wa miti” alisema Bw. Simon Mluge mmoja wa wadau kutoka DCLF.
Kupitia mradi wa Reli ya Kiwango cha kimataifa (SGR) Shirika la Reli Tanzania limekuwa mdau mkubwa wa utunzaji wa mazingira ambapo treni za kisasa zinazotumia umeme zimekuwa zikichangia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.

