Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MRADI WA TIRP II KUONGEZA UFANISI WA RELI YA ZAMANI


news title here
18
January
2026

Shirika la Reli Tanzania linaendelea na awamu ya pili ya mradi wa ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya reli ya zamani ( Tanzania Intermodal Rail Development Project Phase II - TIRP II) kilomita 970 kutoka Dar es salaam - Isaka ( Shinyanga).

Mradi huu unaofadhaliwa na Benki ya Dunia utagharimu kiasi cha dolla za Kimarekani milioni 200 sawa na bilioni 500 za Kitanzania umelenga

Kuimarisha miundombinu ya reli , kuongeza ustahimilivu wa miundombinu kuhimili mabadiliko ya hali ya hewa, kuongeza ufanisi katika uendeshaji , kupunguza gharama za usafirishaji na kukuza biashara.

Aidha, mradi huu utajumuisha ukarabati wa njia ya reli yenye urefu wa kilomita 392.4 na madaraja 171 ili kuiongezea reli uwezo wa kubeba mzigo kutoka tani 15 ekseli moja kabla ya ukarabati mpaka tani 18.5 kwa ekseli moja baada ya ukarabati.

Awamu hii ya pili ya mradi wa TIRP II inalenga kuimarisha usalama katika makutano ya reli na barabara kwa kufunga mifumo maalumu ya kuongoza magari na treni na pia kuimarisha uwezo wa miundombinu ya reli kustahimili changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi hasa katika kipande cha Kilosa, Gulwe na Igandu.

Uboreshaji wa miundombinu ya reli ya zamani utapelekea uanzilishwaji wa mfumo wa kuruhusu waendeshaji binafsi kuingiza treni zao kwenye miundombinu ya reli ( open Access) kama njia ya kushirikisha sekta binafsi kukuza uchumi.

Wakati huohuo katika TIRP ll, TRC itashirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji( NIRC), katika mradi wa ujenzi wa mabwawa sita (6) ya Dabalo, Hombolo, Buigiri, Ikowa, Kimange na Kidete katika wilaya za Kilosa, Mpwapwa na Chamwino ndani ya bonde la maji Kinyasungwe ambayo yatatumika kudhibiti mafuriko.

Ujenzi wa mabwawa haya unatarajiwa kuzinufaisha kaya takribani 50,000 kupitia kilimo cha umwagiliaji, uvuvi na ufugaji na kupunguza shughuli zinazochochea uharibifu wa mazingira.

Kupitia kukamilika kwa mradi wa TIRP II muda wa safari kutoka Dar es Salaam - Isaka utapungua kutoka masaa 50 hadi 30, usafirishaji wa makontena ya mizigo yataongezeka kutoka makonte 400 kwa mwaka hadi 6,000 kwa mwaka na mwisho ufanisi katika upakiaji na ushushaji mizigo utaongezeka kutoka masaa 10 hadi 4 kwa treni moja.

Katika kipindi cha utekelezaji wa mradi wa ukarabati na uboreshaji miundombinu ya reli ya zamani kutakuwa na fursa za ajira za moja kwa moja takriban 3,000 na wanufaika wa moja kwa moja 857, 519 na wasio wa moja kwa moja milioni 3.5 wakiwemo wakazi, sekta za kiuchumi, wateja na wazalishaji .

Utekelezaji wa mradi huu ulianza Machi 2025 na unatarajiwa kukamilika Disemba 2029 ambapo takribani kilomita 577.6 zimeshakamilika na kilomita 392.4 zinaendelea na ujenzi.