ZAIDI YA BILIONI MOJA KULIPA FIDIA KWA WANANCHI MKOANI SHINYANGA
August
2023
Shirika la Reli Tanzania linaendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliotwaliwa maeneo yao kupisha mradi wa ujenzi wa reli yenye kiwango cha kimataifa – SGR kipande cha Mwanza - Isaka, mkoani Shinyanga Agosti 2023.
Zaidi ya Shilingi Bilioni moja zinaendelea kulipwa kwa lengo la kutwaa maeneo na kukabidhi kwa mkandarasi ili aweze kuendelea na shughuli za ujenzi. Wananchi Zaidi ya 1,400 waliopisha mradi wa SGR wanatarajiwa kulipwa fidia katika maeneo ya Malya, Mwalugoye, Mantare, Libaga, Nyamatala, Azimio, Ngeleka, Negezi, Mwagala, Fela, Kahama, Iboja, Kwimba, Misungwi na Maswa.
Maeneo yaliyotwaliwa ni kwaajili ya ujenzi wa tuta la reli yenye kiwango cha kimataifa na miundombinu mingine ikiwemo stesheni, vivuko na madaraja. Ujenzi wa SGR Mwanza – Isaka umefikia zaidi ya asilimia 35 ambapo kukamilika kwa mradi kutasaidi kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.
Zoezi la ulipaji fidia linafanyika kwa ushirikiano wa timu ya maafisa kutoka TRC, viongozi wa mitaa na vijiji husika pamoja na maafisa wa benki ambao wanawahudumia wananchi kupata huduma ya kuweka fedha pindi wananpopokea fidia zao.
Mmoja kati ya wananchi waliopokea fidia katika mtaa wa Lubaga mkoani Shinyanga Bi. Anna Sayi amesema kuwa zoezi la malipo ya fidia limeenda vizuri, wananchi wamewe kupata stahiki zao kwa utaratibu mzuri ambapo kabla ya kupata hundi za malipo ya fidia wananchi walifahamishwa kuhusu utaratibu wa malipo, kubwa zaidi ameshukuru utaratibu uliowekwa kuwarahisishia wananchi kupata huduma za kibenki wakati wa zoezi bila ya kuhitajika kwenda benki.
Mwenyekiti wa kijiji cha Iboje Bwana Hamisi Paschal Mihambo kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha
iboje ameishukuru Serikali kwa kutekeleza ahadi ya kulipa fidia wananchi wote ambao maeneo yao yametwaliwa kupisha mradi wa SGR, pia ameahidia kuendelea kutoa ushirikiano na kuwahamaisha wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha huduma ya usafiri nchini.
“Kwakweli tunaishukuru Serikali kwa kulipa fidia, zoezi hili sio geni kijijini kwetu na wananchi wamekuwa wakitoa ushirikiano kuanzia zoezi la uthamini hadi fidia” aliongeza bwana Hamisi
Mhandisi wa Mradi wa SGR Mwanza – Isaka Bwana Justin Castory amesema kuwa fidia inayolipwa ni kwaajili njia kuu na maeneo ya nyongeza ambayo yanahusisha makaburi, mashamba viwanja na mali nyingine zisizohamishika ikiwemo nyumba na mazao.