Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​ZAIDI YA ABIRIA 1,500 WATUMIA USAFIRI WA TRENI KUTOKA DAR- ARUSHA


news title here
24
December
2021

Shirika la Reli Tanzania linaendelea na huduma za usafiri wa treni katika mikoa ya Kaskazini kutoka Dar es Salaam, Moshi hadi Arusha ambapo zaidi ya abiria 1,500 wameondoka na treni ya Deluxe yenye behewa 20 jijini Dar es Salaam kuelekea Arusha, Disemba 24, 2021.

Kaimu mkurugenzi wa uendeshaji wa huduma kutoka TRC Bw. Focus Sahani amesema kuwa kutokana na muitikio wa wateja kuongezeka shirika limeongeza behewa ili kuhakikisha kila mwananchi amepata huduma.

“Leo tumefunga takribani behewa ishirini na pia safari zimeongezeka kulikuwa na treni ya Jumatatu na Ijumaa ila tumeweka treni ya Jumatano ambayo huwa na behewa kumi“ alisema Bw. Sahani.

Aidha Bw. Sahani alisema kuwa watu wamevutiwa sana na huduma zinazotolewa na TRC kwa kusafirisha abiria kwa bei nafuu zaidi na kupata huduma mbalimbali zenye uhitaji kwa wananchi ikiwemo huduma ya chakula na vinywaji ndani ya treni.

Pia Bw. Sahani ameeleza kuwa TRC inahakikisha inatoa huduma bora kwa wananchi hivyo wajitokeze kwa wingi katika msimu huu wa sikukuu.

“Tunatarajia hivi karibuni kutakua na huduma za treni za umeme, hivyo kwa juhudi zetu wafanyakazi na serikali yetu hatutawaangusha” alisema Bw. Sahani.

Hata hivyo Bw. Sahani amewaasa wananchi kuendelea kuitunza na kuilinda miundombinu ya reli ili kuendelea kupata usafiri wa haraka na nafuu zaidi kwa upande wa abiria pamoja na mizigo.

Naye Mkuu wa kitengo cha Habari na Uhusiano kutoka TRC Bi. Jamila Mbarouk ameeleza kuwa usafiri wa treni ni usafiri bora kwani abiria hupata fursa ya kuona mandhari nzuri pindi anaposafiri ambao ni sehemu ya utalii wa ndani.

“Kusafiri na treni ni zaidi ya safari, hivyo ni muhimu kutumia usafiri wa treni na kuufurahia” alisema Bi. Jamila.

Mmoja wa abiria waliokuwa wakisubiri kusafiri katika Stesheni ya Kamata Bw. Patric Mdoe amesema kuwa usafiri wa treni ni moja kati ya usafiri anaopendelea kutumia na familia hasa katika kipindi hiki cha sikukuu sababu ni nafuu zaidi na pia unaowezesha kupata nafasi za kulala.

TRC inatoa huduma kwa wasafiri kutokana na kuwa na treni ya kawaida na treni ya delux na pia kuwa daraja tofauti zilizomo ndani ya treni ambapo kuna daraja la pili kulala, daraja la pili kukaa pamoja na daraja la tatu kukaa.

Tanzania Census 2022