WAZIRI WA UCHUKUZI ZAMBIA ATEMBELEA MRADI WA SGR

July
2022
Shirika la Reli Tanzania - TRC limepokea ugeni wa Waziri wa Uchukuzi kutoka nchini Zambia na kutembelea mradi wa reli ya kisasa - SGR kutoka Dar es Salam hadi Kwala mkoani pwani hivi karibuni Julai, 2022.
Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka TRC Bw. Focus Sahani amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuona jinsi Tanzania inavyotekeleza mradi huo wa kimkakati wa ujenzi wa reli ya kisasa utakaorahisisha usafirishaji nchini pamoja na nchi jirani kwaajili ya kibiashara hasa usafirishaji wa mizigo mikubwa.
“Tumejaribu hii treni ya mkandarasi kutoka Stesheni ya Dar es Salaam hadi Kwala mkoani Pwani ambapo tumetumia saa moja na dakika arobaini na tano“ alisema Bw. Sahani.
Pia Bw. Sahani ameeleza kuwa mradi huo wa SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia hatua ya mwisho ambapo ujio wa waziri huyo wa Uchukuzi kutoka Zambia utaleta tija kwa nchi za Afrika katika kujenga miundombinu itakayoleta urahisi wa usafirishaji wa magari pamoja na mizigo barani Afrika.
“Lazima tuweke njia bora za usafirishaji katika bara letu la Afrika pamoja na ukanda wa SADC” alisema Bw. Sahani.
Naye Waziri wa Uchukuzi kutoka nchini Zambia Mhe. Frank Tayali amesema kuwa nchi ya Tanzania imefanya kazi kubwa kupitia mradi huo wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa kumaliza kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro na kuendeleza kipande cha pili Morogoro - Makutupora pamoja na vipande vingine ikiwemo kipande cha tatu na kipande cha tano.
“Tunategemea kuona awamu nyingine ambapo Tanzania imeifikia DRC kupitia ujenzi wa miundombinu ya reli“ alisema Mhe. Tayali.
Hata hivyo Mhe. Tayali alieleza kuwa mradi huo wa kimkakati ni uwekezaji mkubwa wa ukuaji wa uchumi nchini hasa nchini Zambia kwa usafirishaji wa madini ya Kopa katika nchi za Afrika.
“Tunawekeza ndani ya miaka kumi ijayo tuwe tunazalisha madini ya Kopa kutoka tani 1000 hadi tani bilioni 3” alisema Mhe. Tayali.
Aidha, Mhe. Tayali ameipongeza nchi ya Tanzania kwa kuendelea kujikita na ujenzi wa mradi huo wa kimkakati wakishirikiana na kampuni ya mkandarasi kutoka nchini Uturuki Yapi Merkezi.
“Nimefurahishwa sana na nilichokiona kwenye mradi huu kutoka Dar es Salaam hadi Kwala na spidi ya treni kuwa nzuri sana na pia nawashukuru sana kutuonyesha maendeleo ya mradi huu“ alisema Mhe. Tayali.
Pia Mhe. Tayali alieleza kuwa Tanzania na Zambia itaendelea kushirikiana katika masuala ya usafirishaji kwa kusafirisha abiria wa nchi hizo pamoja na mizigo.
Tanzania na Zambia ni nchi ambazo zinaendeleza ushirikiano katika masuala ya usafirishaji kupitia miundombinu ya reli ikiwemo reli ya TAZARA inayotoka Tanzania hadi Zambia hivyo mradi wa SGR utaleta tija kwa nchi hiyo kuona namna gani ya kuendelea kushirikiana na kuona fursa mbalimbali zitakazopatikana baina ya nchi hizo mbili.