WAZIRI WA UCHUKUZI AKAGUA UJENZI WA VIVUKO VYA SGR
May
2024
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amefanya ziara Shirika la reli Tanzania – TRC kuanzia Stesheni ya reli ya kiwango cha kimataifa – SGR ya Tanzanite hadi Banana jijini Dar es Salaam mnamo Mei 24, 2024.
Dhima ya ziara ni kuangalia maendeleo ya mradi wa SGR na utayari katika kuelekea kuanza huduma za safari za treni ya kiwango cha kimataifa kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma kuona namna Shirika lilivyojipanga katika kutekeleza ahadi ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuanza safari za treni ya abiria mwezi Julai 2024.
Waziri Mbarawa amezungumzia maendeleo kwenye SGR upande wa treni ya kisasa inayotumia nishati ya umeme (Eelectric Multiple Unit - EMU) ambapo matayarisho yanaendelea ili iweze kufanyiwa majaribio, pia upande wa njia ya treni ambayo inaingia bandarini kwa ajili ya kuchukua mizigo.
“Mahandaki yamekamilika kilichobaki ni kuweka tuta kwaajili ya treni” ameongea Mhe. Mbarawa
Aidha, Waziri wa Uchukuzi alieleza kuwa Vivuko vyote vinatakiwa kukamilika tarehe 10 Juni kikiwemo cha Vingunguti, Airport na Gongo la Mboto ambavyo vipo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi kama uwekaji wa lami, kushindilia vifusi na kuweka uzio wa pembeni ili kuwezesha safari za awali kupitisha treni za abiria Dar es Salaam – Morogoro ifikapo tarehe 14 Juni 2024.
“Tumejipa muda wa kutosha ili kuhakikisha mifumo yote ipo sawa kwenye tiketi na uendeshaji ili kuondoa changamoto zote na kufanya mambo kuwa sawa kabla ya safari za Dar es Salaam - Dodoma kuanza rasmi tarehe 25 Julai 2024” ameeleza Prof. Mbarawa
Pia Waziri Mbarawa ameongelea upande wa nauli za treni za abiria ambapo mchakato wa kupanga bei unasimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini - LATRA ambapo bei elekezi zitakazowekwa zitazingatia hali za Watanzania.
“Hii itakuwa Treni ya mfano tunawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kupanda Treni hii” amesema Waziri wa Uchukuzi Mhe. Mbarawa
Naye, Mkurugenzi Mkuu TRC amezungumzia kazi zilizosalia kwa kipande cha kwanza Dar es Salaam – Morogoro ambapo kuna ukamilishaji wa vivuko vya juu vitatu, vivuko viwili vinatarajiwa kukamilika Mei 31 na kingine Juni 10, ukamilishaji wa mageti kwenye uzio, majaribio ya mifumo ya TEHAMA, ishara na mawasiliano. Kwa upande wa njia ya kuelekea bandarini ujenzi wa tuta na kivuko kilichopo barabara ya Nyerere kitakuwa tayari tarehe 30 Juni na maendeleo ya majaribio kwa vitendea kazi vipo kwenye hatua nzuri.
“Mabehewa 28 na vichwa 3 vya treni vimekamilika katika hatua ya majaribio na vipo tayari kwa uendeshaji na majaribio yanaendelea kwa mabehewa 14 na Seti 1 ya EMU na vichwa 6” ameongezea Mkurugenzi Kadogosa
TRC chini ya Wizara ya Uchukuzi inaendelea kusimamia mradi wa SGR katika kufikia utekelezaji wa kuanza safari za Dar es Salaam hadi Dodoma ifikapo Julai 25, 2024 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan la safari za treni ya abiria ifikapo Julai 2024.