WAZIRI WA MIUNDOMBINU WA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO ATEMBELEA MRADI WA SGR

November
2022
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Tanzania Prof. Makame Mbarawa akiongozana na Waziri wa Miundombinu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - DRC Alexis Gusaro pamoja na viongozi wengine kutoka DRC wametembelea jengo la Stesheni ya SGR jijini Dar es Salaam, Novemba 2022.
Prof. Makame Mbarawa amesema lengo la ziara ya Waziri wa Miundombinu DRC ni kuendeleza ushirikiano wa Kongo na Tanzania katika nyanja za kiuchumi na uhusiano kupitia miundombinu mizuri ikiwemo reli na bandari baina ya nchi hizi mbili.
Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi wa DRC Mhe. Alexis Gusaro akiongozana na Waziri mwenza Cherubin Senga wametembelea jijini Dar es Salaam kwaajili ya kusaini makubaliano ya ujenzi wa miundombinu ya Reli, Meli, Bandari na Barabara kati ya nchi hizo.
Mheshimiwa Alexis Gusaro amesema kuwa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR utasaidia shughuli za biashara kati ya Tanzania na Kongo kwa kuwezesha kusafirisha mizigo kwa haraka na usalama zaidi, pia ameipongeza TRC kwa kuweza kuweka mipango ya kujenga reli itakayokua inaunganisha Kongo na Tanzania.
"DRC tuna madini mengi tunaweza kusafirisha madini na mizigo mingine kutoka Kongo kuja Tanzania kupitia njia ya reli na kutoka Tanzania kwenda Kongo" alisema Mheshimiwa Alexis Gusaro.
Gavana wa jimbo la Tanganyika nchini Kongo Bi. Julie Mwayuma ameipongeza Tanzania kwa mradi mkubwa wa SGR na wanategemea mambo mazuri zaidi pindi SGR itakapofika Karemii mji wa Tanganyika ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo ya biashara.
Ziara hii ya makubaliano ya ujenzi wa miundombinu ya Reli, Meli, Bandari pamoja na Barabara itachochea fursa ya usafirishaji wa bidhaa za biashara kwenda Kongo kwakua inaitegemea Tanzania katika uingizaji wa mizigo kutoka nchi mbalimbali kupitia bandari na kuisafirisha kwa kutumia Reli na Barabara hadi Kongo.