Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WAZIRI WA MIUNDOMBINU WA BURUNDI ATEMBELEA MRADI WA SGR


news title here
29
November
2022

Shirika la Reli Tanzania – TRC limepokea ugeni wa Waziri wa Miundombinu kutoka nchini Burundi Mhe. Dieudonne Dukundane kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam – Morogoro katika stesheni kuu ya SGR jijini Dar es Salaam hivi karibuni Novemba, 2022.

Kaimu Mkugugenzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sheria kutoka TRC Bw. Vicent Tangoh ameeleza kuwa TRC imeshasaini mkataba wa makubaliano ambayo yataweza kuunganisha reli kutoka Tanzania hadi Burundi mpaka Congo ambapo njia hiyo ya reli italeta urahisi wa usafirishaji wa madini na mizigo mbalimbali.

“Burundi ni wenzentu hivyo lazima wapewe wataalamu sababu tumeshapiga hatua kubwa kama unavyoona sehemu kubwa ya ujenzi wa SGR tunatumia wataalamu wetu wa ndani na tayari tumemaliza kipande cha kwanza na cha pili kipombioni kumalizika” alisema Bw. Tangoh.

Pia Waziri wa Miundombinu wa Burundi Mhe. Dieudonne Dukundane alisema kuwa kipande cha reli ya kisasa cha Tanzania kuingia Burundi kitatokea Uvinza na kupitia Msongati eneo ambalo lina madini mengi na pia Kitega na kufika Congo.

“Sisi Burundi tunajitayarisha kwa kuanza kukusanya fedha pamoja na kuhesabu makazi ya watu na vitu vitakavyoharibika ili kuweza kulipa watu watakao athiriwa na mradi utakaojengwa” alisema Mhe. Dukundane.

Aidha Mhe. Dieudonne Dukundane aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kuweza kusimamia mradi huo wa kimkakati ambao utasaidia nchi za jumuia ya Afrika Mashariki kuweza kushindana na kushirikiana kibiashara na kiutaalamu.

«Tumepata majibu mazuri kuwa Tanzania ipo taari kuwapokea vijana wetu ili waweze kujifunza na tumefurahi sana» aliongezea Mhe. Dukundane.

Mradi wa SGR umeendelea kuwa chachu ya kuwezesha nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati kuendelea kuungana katika kuleta mikakati mbalimbali ya kukuza miundombinu ya reli pamoja na kutanua wigo wa kibiashara.