Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WAZIRI MKUU; TRENI ZA RELI YA KISASA KUANZA KUTOA HUDUMA MAPEMA 2021


news title here
19
November
2020

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali inatarajia kukamilisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha Dar es Salaam – Morogoro na kuanza kutoa huduma mapema mwaka 2021 Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo alipofanya ziara ya ukaguzi kuona maendeleo ya mradi huo Novemba 18, 2020.

Lengo la ziara hiyo ni kuona maendeleo ya kazi na kuwaonesha watanzania kuwa utekelezaji wa kazi za miradi unaendelea kama ilivyokuwa awali.

“Mradi huu ni mkubwa na wa mkakati, kama mnavyojua mradi huu una awamu mbili lakini nimefurahi kwa sababu mpaka sasa tumefikia hatua nzuri sana, leo nimekuja kukagua kituo kikubwa cha hapa Morogoro, nilishafanya hivyo kwenye jengo la Tanzania Dar es Salaam lakini pia nitakwenda Kwala” alisema Mhe. Waziri Mkuu

Mhe. Kassim Majaliwa amefanya ziara hiyo ikiwa ni ya kwanza tangu kuapishwa kwake kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya uteuzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli hivi karibuni kufuatia uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020 ambapo Dkt. Magufuli alishinda nafasi ya urais.

Aidha, Mhe. Waziri Mkuu amekagua jengo la Stesheni ya Reli ya Kisasa - SGR mkoani Morogoro pamoja na ujenzi wa kituo cha kupanga treni za mizigo sambamba na ujenzi wa Karakana ya Behewa na Vichwa vya treni za kisasa katika eneo la Kwala, Mhe. Waziri amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya Mradi wa SGR pia amewapongeza wafanyakazi na menejimenti ya TRC ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Prof. John Kondoro na Mkurugenzi Mkuu Ndugu Masanja Kadogosa.

“Nimepita huku ndani nimeona kazi pamoja na taarifa, nimeridhishwa na kasi ya ujenzi, Yapi Merkezi fanyeni kazi kwa sababu watanzania wanatamani kuona treni zikianza kutembea kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro ifikapo mwezi Aprili” alisema Mhe. Majaliwa

Mkurugenzi Mkuu Ndugu Masanja Kadogosa aliuelezea ujio wa Waziri Mkuu kukagua mradi wa SGR kwa kusema kuwa “Serikali inaungalia mradi huu kwa jicho la karibu, sisi menejimenti na bodi yetu tunapaswa kujipanga vizuri kwa sababu huu ni mradi wa kimkakati lakini pia ni heshima kutembelewa na viongozi wakuu, sisi kama viongozi kazi yetu ni kuwasimamia wakandarasi kuhakikisha inapofika Aprili 2021 treni zinaanza kutembea”

Mkurugenzi Mkuu ametaja baadhi ya changamoto ambazo zimepelekea kuchelewa kukamilika kwa mradi huo ikiwemo mripuko wa ugonjwa wa Korona ambao ulisababisha baadhi ya vifaa kutopatikana kutokana na kufungwa kwa biashara katika baadhi ya nchi kwa muda mrefu, lakini kwa sasa vifaa vimeanza kuingia bandarini, kazi zinaendelea na Mkandarasi tayari ametandika reli kwa kipande cha zaidi ya Kilometa 145 kati ya 200.

Juhudi za kuimarisha sekta ya miundombinu ya reli nchini zinatekelezwa na serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inayoongozwa na Jemedali Dokta John Pombe Magufuli kwa ajili ya watanzania. TRC inaendelea kuwakumbusha wananchi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mh.Rais Dokta John Pombe Magufuli.