WANANCHI MKOANI MWANZA WAPATA ELIMU KUHUSU USALAMA WA MRADI WA SGR
March
2026
Shirika la Reli Tanzania (TRC) linaendelea na kampeni ya kuhimiza wananchi waishio karibu na mradi wa Standard Gauge Railway (SGR) kipande cha tano Isaka - Mwanza kulinda miundombinu ya reli kutokana na umuhimu wake mkubwa kwa maendeleo ya uchumi na usafirishaji.
Katika mikutano ya hadhara, maafisa kutoka TRC walisisitiza kwamba mradi wa reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) ni mali ya Taifa ambayo inapaswa kulindwa na kila mwananchi. Walisema kwamba vitendo vya uharibifu kama kukata uzio, nyaya za umeme, au kuvuka maeneo yasiyo rasmi yanahatarisha usalama wa reli na mradi.
“Reli ya SGR ni mali ya Watanzania wote, kila mmoja ana wajibu wa kuilinda kwa manufaa ya Taifa na vizazi vijavyo.” alisema Mhandisi Mradi, Bi. Nastra Chusi.
Afisa wa ulinzi na usalama wa reli Bwana Richard Msungu, aliwahimiza wananchi kuhakikisha shughuli zao za kila siku ikiwemo kilimo, ufugaji, na biashara zinafanywa nje ya hifadhi ya reli ili kuhakikisha usalama wao na wa mradi mzima.
Aidha, akikumbusha Sheria ya Reli namba 10 ya mwaka 2017 na kanuni za adhabu kuhusu uharibifu wa miundombinu, Mwanasheria kutoka TRC Bwana Hamimu Nkoleye alisisitiza kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayefanya vitendo vitakavyohatarisha usalama wa reli au mradi.
Kampeni hiyo inafanyika ikiwa siyo tu kuhusu kulinda miundombinu bali pia ni kuelekeza wananchi kuwa sehemu ya mafanikio ya mradi wa SGR, unaotarajiwa kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo, kupunguza gharama za usafirishaji, na kuchochea maendeleo ya kibiashara katika mikoa mbalimbali.
Ujumbe huo ulikua wa wazi kwamba reli ya SGR sio tu mradi wa kisasa wa usafirishaji bali ni rasilimali ya Taifa ambayo inahitaji ushirikiano wa kila mtu ili kudumu salama na kutoa huduma kwa vizazi vijavyo.

