Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WAZIRI MKUU MHE.KASSIM MAJALIWA ASHUHUDIA MAJARIBIO YA KWANZA TRENI YA SGR KUTOKA DAR ES SALAAM- DODOMA


news title here
22
April
2024

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ashuhudia majaribio ya Kwanza ya treni ya SGR kutoka Dar Es Salaam- Dodoma , Aprili 21, 2024.

Treni hiyo ya Kwanza ya majaribio imebeba viongozi mbalimbali wa Serikali ,viongozi Wakuu WA dini Tanzania,maofisa wa Taasisi mbalimbali za Serikali ,wasanii pamoja na waandishi wa vyombo vya habari imesafiri kutoka Dar Es Salaam kwenda makao mkuu ya nchi Dodoma kwa ajili ya sala maalumu ya kuliombea Taifa kuelekea kilele cha miaka sitini ( 60) ya Muungano wa Tanzania.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa safari hiyo ya majaribio Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi WA dini ili kuendelea kudumisha Amani ,Upendo na kujenga nchi yetu.

"Leo ni siku ya kihistoria kuelekea kilele cha miaka sitini ya Muungano wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania,uzinduzi wa njia ya Reli kutoka Dar Es Salaam - Dodoma inaonesha thabiti hatua chache zilizobaki ili tuanze safari rasmi, na Jambo la Furaha zaidi kundi la Kwanza kuzindua safari hii ni viongozi wa dini" Amesema Waziri Mkuu.

Aidha , Waziri Mkuu ameongeza kuwa safari ya viongozi WA dini kwa treni ya Kwanza ya majaribio kutoka Dar Es salaam - Dodoma ni kuendeleza tunu ya Taifa ya Amani iliopo nchini kutokana na watanzania wengi kuwa waumini na Imani za dini mbalimbali .

"Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan anawahasa viongozi WA dini kuendelea kuliombea Taifa kwani Taifa linajengwa kwa misingi imara ya dini, na Serikali inazidi kuheshimu dini kwani inamchango mkubwa kwa Taifa na maendeleo hayawezi kupatikana bila uwepo WA dini" Amesema Mhe.Majaliwa.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe.David Kihenzile amewahakikishia watanzania kuwa ifikapo mwezi Julai mwaka huu safari za treni za SGR zitaanza kusafirisha abiria rasmi kutoka Dar Es Salaam mpaka Dodoma rasmi.

" Naomba nichukue fursa hii kuwahakikishia watanzania kuwa kwa majaribio haya tulioanza Leo, ifikapo mwezi Julai mwaka huu ,treni zetu za SGR zitaanza kusafirisha abiria rasmi kutoka Dar Es salaam - Dodoma bila shaka yoyote" Alisema Mhe.Kihenzile.

Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ameeleza kuwa katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania miongoni mwa mafanikio ya Serikali ni ujenzi wa Reli ya kimkakati ya kimataifa ya SGR ambao unatekelezwa kwa gharama ya Dola za Kimarekani Bilioni 10.01 sawa na shilingi za kitanzania trilioni 23.3 na utekelezaji wake uko katika hatua mbalimbali.

"Kazi ya majaribio inaendelea kufanyika kwa vichwa na mabehewa ya abiria ,tunasubiri Sana mabehewa ya mizigo kwani huko ndipo kwenye faida na fursa za uchumi zaidi" Amesema Ndugu Kadogosa.

"Tunashukuru Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa hatua hii,kama viongozi WA dini tunaendelea kuiombea nchi na Serikali kwa ujumla katika utekelezaji wa majukumu yake" Amesema Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kikutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Mashariki na Pwani Usharika wa Makongo George Fupe.

Shirika la Tanzania linajiandaa kuanza kwa shughuli za uendeshaji treni za SGR na mpaka sasa tayari inepokea mabehewa 65 Kati 89 ya abiria na vichwa 9 Kati ya 19 vya kuvuta behewa za abiria na mizigo na seti moja kati ya 10 za treni ya kisasa (EMU).