Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WAZIRI MKUU MAJALIWA ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA RELI YA KISASA MOROGORO – MAKUTUPORA


news title here
24
November
2022

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR Morogoro – Makutupora katika jengo la stesheni kuu ya SGR jijini Dodoma, Novemba 24, 2022.

Lengo la ziara ya Waziri Mkuu ni kutembelea miradi ya kimkakati kwa lengo la kuona maendeleo ya utekelezaji wake ambapo pamoja na kutembelea jengo la Stesheni ya SGR ambalo ujenzi wake umefikia 32%, Mhe. Waziri pia ametembelea jengo la ofisi ya makao makuu linalojengwa jirani na jengo la stesheni.

“Watanzania wenzangu naendelea na ziara za kukagua miradi yetu nchini na mradi huu wa SGR ni mmoja kati ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini, kupitia ziara hii watanzania watajua mradi wao mkubwa umefikia hatua gani” alisema Waziri Mkuu

Waziri Mkuu amesema kuwa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu TRC inaonesha maendeleo ya mradi wa reli ya kimataifa ambapo alipata fursa mara kadhaa ya kukagua mradi huo Dar es Salaam hadi Mwanza ambapo ameridhishwa na kasi ya maendeleo yake na kuipongeza Wizara, TRC, Wakandarasi na Wafanyakazi wote kwa usimamizi mzuri.

“Nimeingia kwenye jengo letu hili ambalo ni kubwa kuliko majengo yote ya Shirika la Reli ambalo ujenzi wake umefika 32%, wakati jengo hii la makao makuu limefikia 92% sina mashaka na tarehe za ukamilishaji” alisitiza Mhe. Majaliwa

Aidha, Mhe. Waziri amewataka watanzania wanaofanya kazi katika mradi kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanapata ujuzi utakaowawezesha kufanyakazi ya kujenga na kukarabati reli mara baada ya wakandarasi kuondoka nchini.

Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. Atupele Mwakibete ameeleza kuwa vipande vyote vitano kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza vina wakandarasi, kazi inaendelea na hakuna mkandarasi anayeidai Serikali, jumla ya Trilioni 7 zimekwishalipwa. Atupelea ameongeza kuwa mapema mwaka 2023 huduma za uendeshaji wa reli ya kisasa zitaanza kwakuwa tayari behewa zimeanza kuwasili nchini.

Kadhalika Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha wanajipanga kuleta wawekezaji katika maeneo ya stesheni na pembezoni mwa reli ya SGR pamoja na kuleta huduma muhimu katika eneo la Stesheni kuu ya Dodoma ili kurahisisha usafirishaji na shughuli za kiuchumi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Kondoro ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono uboreshaji wa miundombinu ya reli pia ameongeza kuwa zipo changamoto kadhaa zilizopelekea kuchelewa kwa mradi ikiwemo zoezi la kuhamisha nyumba, shule na baadhi ya miundombinu hususani katika jiji la Dar es Salaam. Prof. Kondoro aliongeza kuwa janga la UVIKO19 nalo lilichangia kwa kiasi kikubwa kuchelewa kwa mradi

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Masanja Kadogosa ametoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa SGR ambao unatekelezwa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa vipande vitano ambavyo ujenzi wake umefikia 97.63 Dar es Salaam – Morogoro, Morogoro – Makutupora 90.02%, Makutupora – Tabora 2.31%, Tabora – Isaka kazi ya maandalizi inaendelea huku kipande cha Mwanza – Isaka kikiwa kimefika 16.71.

Kadogosa ameongeza kuwa “ mpaka kufikia Machi 2026 tutakuwa tumeshamaliza kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza”

Akielezea uwezo wa Stesheni ya SGR Dodoma, Kadogosa amesema kuwa Stehsni ya Dodoma itakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria Milioni 1.1 kwa mwaka, maduka kupokea mabasi 165, maegezo ya magari madogo 20, maegezo ya watu maalum (VIP) 20, maegesho ya magari ya baishara 15, maegezo ya pikipiki na baiskeli zaidi ya 50 na maegezo 10 ya watu wenye ulemavu.