Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WAZIRI MKUU MAJALIWA AFANYA ZIARA KATIKA MRADI WA SGR MWANZA - ISAKA


news title here
16
October
2022

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amefanya ziara kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR Mwanza – Isaka Oktoba 16, 2022.

Lengo la ziara ni kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali katika mikoa ya kanda ya ziwa ukiwemo mradi wa SGR kipande cha tano Mwanza – Isaka (km 341) ambao ujenzi wake umefika zaidi ya asilimia 14.

“Ziara hii nimeanza kwenda daraja letu linalounganisha Kigongo na Busisi ambalo pia ni la kimkakati linaendelea vizuri, nimekuja hapa Misungwi eneo la Fela kukagua ujenzi wa reli hii ya kimataifa ambayo inajengwa kutoka Mwanza hadi Isaka” amesema Mhe. Majaliwa

Waziri Mkuu alipata fursa ya kuona mabango ya picha za kazi mbalimbali zilizofanyika ikiwemo ujenzi wa tuta, madaraja, makalavati na kambi za ujenzi. Pia ameona picha zinazoonesha muonekano wa stesheni za SGR zitakazojengwa katika kipande cha tano.

“Hapa kwenu Fela wilaya ya Misungwi ndio itakuwa bandari Kavu, mizigo yote inayotoka Dar es Salaam itashuka hapa na mizigo inayotoka Uganda na kwengineko italetwa hapa kupakiwa kwenye treni kwenda Dar es Salaam” amesema Waziri Mkuu

Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Godfrey Kaselenya amemshukuru Mhe. Waziri Mkuu kwa kutembelea mradi wa SGR katika kituo cha Fela. Ameeleza kuwa reli ya SGR itakapokamilika kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza itakuwa na urefu wa kilometa 1,219 na muda wa safari utapungua hadi saa 8 kutoka saa 18 hadi 20 za sasa.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu TRC ambaye ni Mkurugenzi wa Rasilimali watu na utawala Bi. Amina Lumuli ametoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa SGR kipande cha tano ambayo ilieleza kuwa mradi wa SGR Mwanza – Isaka umefikia 14.12 kufikia mwezi wa tisa. Hivi sasa kazi ya usanifu wa kutengeneza tuta kwaajili ya kulaza reli unaendelea ambapo takribani reli laki tano zitalazwa pamoja na stesheni 10 zitajengwa katika kipande hiko.

Bi. Amina ameeleza kuwa “Mradi huu umetoa ajira takribani 5400 na tutakapokamilisha tutakuwa na wafanyakazi 11,000 hadi 11,000 vilevile mradi utakapokamilika TRC itakuwa na uwezo wa kuajiri zaidi ya wafanyakazi 10,000”

Bi. Amina ameongeza kuwa gharama za mradi kwa vipande vitano kutoka Mwanza hadi Isaka ni zaidi ya 16.67 na kipande cha Mwanza – Isaka 3.12 vilevile Serikali imekwishalipa kwa kazi zilizofanyika kwa zaidi ya Trilioni 6.67, hivyo Serikali haidaiwi kwa kazi zote zilizofanyika hadi sasa.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu kwa niaba ya Shirika la Reli ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, Mawaziri wakiongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi.