Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WAZIRI MKUU ATOA HEKO KWA TRC: AJIONEA KAZI NZURI ILIYOFANYIKA MRADI WA SGR


news title here
22
April
2021

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametembelea mradi wa ujenzi Reli ya Kisasa (SGR) kukagua jengo la Stesheni na ujenzi wa Daraja linalounganisha Stesheni hiyo ikiwa ni ziara ya kufuatilia miradi mbalimbali ya kimkakati inyoendelea kutekelezwa nchini, Aprili 20, 2021.

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Waziri Mkuu amelipongeza Shirika La Reli Tanzania (TRC) kwa kazi nzuri inayofanywa ya kusimamia mradi na kuwataka wafanyakazi wa shirika hilo kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewahakikishia wananchi kuwa mradi huu na mingine ya kimkakati itaendelea na kukamilishwa kama ilivyopangwa.
“Mradi huu tutaendelea kuujenga hadi uishe, tutaendelea na awamu ya pili (Tabora - Kigoma) na ya tatu (Tabora – Mpanda - Karema)” alisema Waziri Mkuu
Aidha, Mheshimiwa Kassimu Majaliwa ameongeza kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi zipo na serikali imejipanga vizuri, hivyo amelitaka Shirika La Reli Tanzania (TRC) kumsimamia mkandarasi vizuri na kuzitumia fedha hizo vizuri.
“Raisi wetu mama Samia Suluhu Hassan amenihakikishia hela ipo na tumejipanga vizuri na kwa utulivu na amani, Serikali yetu haitabadilika, pesa tulizoziweka kwenye mradi zitatumika vizuri” aliongeza Mhe. Waziri Mkuu.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Dkt. Leonard Chamuriho, alitolea ufafanuzi kuhusu kuchelewa kukamilika kwa mradi kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro ni kutokana na kutokukamilika kwa daraja la KM 2.56 linaounganisha Stesheni ya Dar es Salaam kwa lengo la kuepukana na msongamano wa magari na watu katikati ya jiji, hata hivyo Waziri Chamuriho ameeleza kuwa ifikiapo mwezi Agosti treni zitaanza kutembea kuanzia stesheni ya Pugu kuelekea Morogoro.
Katika ziara hiyo Mkurugunzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kadogosa alitoa taarifa ya maendeleo ya mradi kuwa kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kimekamilika kwa 91% ambapo makalavati 248 yameshakamilika kujengwa, madaraja 117 nayo tayari yameshakamilika na matarajio ni kuwa ifikapo Agosti mwaka huu uendeshaji wa treni kutoka Pugu mpaka Morogoro utaanza.
“Mheshimiwa waziri Mkuu, stesheni hii ya Dar Es Salaam imekamilika ,kinachoendelea ni installation ya syatem ya mawasiliano, ulinzi na landscaping, utakapo kuja tena utakuta mandhari nzuri sana,mpaka sasa tuna asilimia 91 imekamilika katika ujenzi huu “ Alisema Kadogosa
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TRC aliongeza kuwa awamu ya pili ya ujenzi wa mradi imekamilika kwa 57.7% na mpaka kufikia mwisho wa mwezi Aprili itakamilika kwa asilimia 60 na ifikapo Agosti mwaka huu kipande cha Morogoro - Makutupora kitakuwa kimeunganishwa na kufikia Februari 28, 2022 kipande hiki kitakuwa kimekamilika.