WAZIRI MKUU ASHUHUDIA RELI ILIYOTANDIKWA, MRADI WA SGR MWANZA – ISAKA WAFIKA 28%
March
2023
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameshuhudia reli iliyoanza kutandikwa katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR Mwanza – Isaka akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu Machi 26, 2023.
Mhe. Waziri Mkuu ametembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia eneo la Nyashimbi hadi Malampaka mkoani Simiyu kwa lengo la kukagua na kuona maendeleo ya mradi wa SGR Mwanza – Isaka uliofikia asilimia 28 huku kazi ya ujenzi wa Stesheni na utandikaji reli ikiwa inaendelea kwa kasi.
“Ziara yangu leo Maswa hapa Malampaka ni kuja kukagua reli ya kiwango cha kimataifa inayoendesha treni kwa kutumia umeme na hapa Malampaka kitajengwa kituo kikubwa cha abiria na mizigo aina zote, hii reli nimeikagua mpaka naingia hapa inaendelea kujengwa viwango vyake ni vya kimataifa na itatumia muda mchache abiria na mizigio kufika hapa” alisema Waziri Mkuu
Waziri Mkuu amewataka wananchi wa kata ya Malampaka kuchangamkia fursa zilizopo katika mradi wa reli ya kisasa pamoja na kituo cha abiria na mizigo kitakachojengwa ili kuwaongezea kipato na kukuza uchumi.
“Niko mkoani Simiyu kwa siku tatu kukagua miradi ya maendeleo inayojengwa nimeona miradi yenu mingi imefikia hatua nzuri, mingine imekamilika imeanza kufanya kazi, nimekuja kuona reli kazi zinaendelea. Reli hii itaweka kituo hapa Malampaka jipangeni hususani katika upimaji ardhi na kutoa hati, hii reli inajengwa kwaajili yenu” alisema Waziri Mkuu
Waziri Mkuu ameeleza kuwa ikiwa ni miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan miradi inaendelea na imefikia hatua nzuri. Malengo ni kukamilisha utekelezaji wa ilani ya CCM angalau kwa asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.
Wananchi wa Malampaka waliohudhuria mkutano wa Waziri Mkuu wamesema kuwa wamefurahishwa na ujio wa mradi wa SGR na wanaamini kuwa utaleta manufaa kiuchumi hivyo wamejipanga kuchangamkia fursa zilizopo na zitokanazo na mradi ikiwemo kujenga nyumba za wageni, viwanda ikiwemo vya kuchambua pamba na kuboresha kilimo kwa kutumia umwagiliaji kwani kutakuwa na uhakika wa usafiri wa mazao kwenda kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.