WAZIRI MKUU ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA MRADI WA UJENZI WA RELI YA KISASA - SGR

May
2020
Waziri mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR alipotembelea awamu ya kwanza ya ujenzi kipande cha Dar es Salaam hadi Kilosa- Morogoro 14 Mei, 2020.
Waziri mkuu amesema kuwa ni hatua kubwa sana iliyofanyika katika ujenzi wa mradi wa SGR ambapo kipande cha kwanza Dar es Salaam- Morogoro cha ujenzi umefikia asilimia zaidi ya asilimia 77.
“Nimeshudia mwenyewe kwa kupanda treni ya majaribio ya wahandisi ili nijiridhishe na ukaguzi wa njia na kiukweli nimeridhika“ alisema Mhe. Majaliwa.
Aidha Waziri Mkuu ameipongeza kampuni ambayo inasimamia ujenzi huo pamoja na kutoa pongezi za dhati kwa Shirika la Reli Tanzania - TRC kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi wa SGR unakamilika kwa uimara na kwa wakati unaostahili kulingana na masharti ya Serikali juu ya ujenzi huo .
Pia Waziri Mkuu alitoa Shukrani zake kwa Mkurugenzi mkuu wa TRC pamoja na kamati nzima ya Bodi ya Shirika hilo kwa kutekeleza maagizo ya wizara pamoja na kutafuta kampuni nzuri kutoka Uturuki ya wakandarasi wa ujenzi wa reli ya kisasa Yapi Markezi.
“Kampuni hii imefanya kazi nzuri kama Serikali ilivyotaka” aliongezea Mhe. Majaliwa .
Waziri alivitaja vyanzo vitatu vya umeme ambavyo vitatumika katika uendeshaji wa treni ya umeme pindi itakapoanza uendeshaji na kusema kuwa vyanzo hivyo ni umeme kutoka bwawa la Mwalimu Nyerere, umeme kutoka kidatu na Mtera na cha tatu ni umeme kutoka Kinyerezi kwa kutumia gesi inayotoka Mtwara .
“ Nimetembea na nimeona tayari nguzo za umeme zimeshatandikwa kati ya nguzo 160, nguzo 154 tayari zimeshatundikwa kwa awamu hii ya kwanza “ alisema Mh Waziri .
Waziri Mkuu amependezwa sana na ujenzi wa vituo vya Station alipotembelea kituo cha Station cha Soga na kusema kuwa ni vituo vyenye viwango na vya kimataifa ambavyo vitazungukwa na huduma mbalimbali za kijamii.
Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Atashasta Nditiye amesema kua hivi karibuni Serikali inatarajia kuja kuzindua safari kipande cha Dar es Salaam- Morogoro kwa kua awamu ya ujenzi katika kipande hicho kiko mbioni kukamilika.
Mhe. Nditiye amesema kuwa kuanza kutumika kwa reli hiyo ya kisasa kutaleta faida kubwa katika nchi ikiwemo ukuaji wa uchumi kwa kutumia mda mfupi na kukamilisha shughuli kwa haraka pamoja na jamii kufaidika katika kutokomeza hadha ya usafiri na kutumia treni ya mwendokasi.
Pia Mkurugenzi Mkuu wa TRC ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema kua changamoto nyingi zinajitokeza ila zinafanyiwa kazi kwa hara kwa leo la kupata ujenzi ulio bora na imara.
Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu amesema kuwa ujenzi huo wa SGR unaenda kwa kasi kwa vipande vyote viwili ya Dar es Salaam - Morogoro na awamu ya pili ya Morogoro - Makutupora.
Juhudi za kuimarisha sekta ya miundombinu ya reli nchini zinatekelezwa na serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inayoongozwa na Jemedali Dokta John Pombe Magufuli kwa ajili ya watanzania. TRC inaendelea kuwakumbusha wananchi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mh.Rais Dokta John Pombe Magufuli.