Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WAZIRI MBARAWA AIPONGEZA TRC KWA JITIHADA ZA HARAKA KUREJESHA NJIA KIDETE


news title here
11
March
2022

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa, ametembelea eneo la reli lililosombwa na maji na kupelekea kusitishwa kwa huduma za usafiri wa reli kupitia reli ya kati, Kidete wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, Machi 10, 2022.

Kipande hicho cha reli kilisombwa na maji Februari 28, 2022 kufuatia daraja la reli lililoko jirani na Stesheni ya Kidete kukatika hali ambayo imepelekea mawasiliano kati ya Dar es Salaam na Mikoa ya Dodoma, Tabora, Mwanza, Katavi na Kigoma kupitia reli ya kati kukatika kwa takribani siku 10.

Akiwa eneo la tukio Waziri Prof. Mbarawa ameshuhudia juhudi za kurudisha mawasiliano zikiwa katika hatua za mwisho kwa ushirikiano kati ya Shirika la Reli Tanzania na Kampuni ya Mkandarasi wa Ujenzi wa SGR, Yapi Merkezi ya nchini Uturuki.

Akieleza kazi iliyofanyika, Mratibu wa Miradi kutoka TRC, Mhandisi Nelson Ntejo amesema kuwa mmomonyoko na wingi wa maji yaliyosababishwa na mvua ulipelekea nguzo za daraja kuanguka na reli kusombwa.

Aidha, Mhandisi Ntejo ameeleza kuwa “ili kurejesha mawasiliano ilibidi kutengeneza njia mbadala yenye urefu wa Mita 660 pamoja na daraja ambalo tumejenga kwa kozi mbili za makaravati”

Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa ameeleza kuwa eneo la Kidete ni sehemu ya Kipande cha reli ambacho hakikufanyiwa ukarabati katika mradi wa Uboreshaji wa Reli ya Kati uliofadhiliwa na Benki ya Dunia.

“kipande hiki kiliachwa kwasababu kulikuwa na wadau ambao waliahidi wangekikarabati lakini baadaye hawakuendelea na mpango huo, lakini kuna upembuzi ambao utafanywa na Benki ya Dunia kwaajili ya kuhamisha njia” alisema Ndugu Kadogosa.

Waziri Prof. Makame Mbarawa baada ya kukagua maendeleo ya kazi ya kurejesha kipande hicho cha njia ya reli, ameeleza kuridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa na wahandisi na vijana wazalendo.

“kwanza nishukuru wote ambao wamefanya kazi usiku na mchana ili kurejesha njia hapa Kidete, siku zote majanga yanatokea lakini jambo muhimu kwa wahandisi na taasisi ni kurejesha huduma kwa haraka, na hiyo ndio iliyotokea hapa, huu ni mfano mzuri, kwahiyo mimi nawapongeza sana, nakushukuru sana Mkurugenzi Mkuu na Shirika kwa Ujumla”

Kukatika kwa kipande hicho cha reli kulipelekea huduma ya Usafiri wa treni kusitishwa kwa muda katika reli ya kati tangu Februari 28 mwaka huu, ambapo kutokana na hatua iliyofikiwa katika jitihada za kurejesha njia ya reli, inategemewa huduma kurejea hivi karibuni baada ya majaribio ya njia kwa kutumia treni ya Mizigo.