Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WATAALAMU MAMLAKA ZA HALI YA HEWA BARANI AFRIKA NA ULAYA WAZURU SGR


news title here
16
September
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC limepokea wajumbe takribani 150 kutoka Mamlaka za Hali ya Hewa Barani Afrika na Mashirika ya Satelite Barani Ulaya kutembelea ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR Septemba 15, 2022.

Wajumbe kutoka nchi zaidi ya 70 kote duniani wakiambatana na mwenyeji wao kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wamefanya ziara ya kutembelea ujenzi wa mradi wa SGR kipande cha Kwanza kutoka stesheni ya Dar es Salaam mpaka stesheni ya Pugu na kujionea maendeleo ya na ujenzi wa mradi huo.

Akiongea wakati wa ziara hiyo Bwana Wilbert Timiza Mubuke Meneja wa Mahusiano ya Hali ya Hewa Kimataifa kutoka Mamlaka ya Hewa nchini ambaye pia ni mkuu wa msafara katika ziara hiyo amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kujionea jinsi gani sekta ya ujenzi wa miundombinu ya miradi mikubwa ukiwemo SGR na sekta ya usafirishaji wa nchi kavu unavyotegemea Mamlaka za Hali ya hewa katika shughuli zake.

"Mojawapo ya sekta inayotumia sana huduma hizo ni sekta ya usafiri wa nchini kavu hasa usafiri wa reli kwahiyo ndio maana tumekuja kuona mradi huu wa SGR kwa namna ambavyo unatumia hali ya hewa" amesema Bwana William Mubuke.

Aidha, Bwana Mubuke ameongeza kuwa baada ya kongamano hilo la 15 la Mamlaka za Hali ya hewa barani Afrika na Shirika la Setelite Barani Ulaya itarushwa setiliti ambayo itakuwa na uwezo wa kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa uhakika na hivyo kuisaidia sekta ya usafirishaji wa reli kuendelea zaidi.

Miongoni mwa wajumbe hao katika ziara hiyo Meneja Mratibu Kongamano la Wataalamu wa Mamlaka za Hewa Afrika Bi. Mariane Diop Kane kutoka nchini Senegal ambaye ni ameeleza kufurahishwa kwake na ujenzi wa SGR ambao utaenda kuunganisha nchi nyingi za Afrika kijamii na kibiashara na kuleta maendeleo ya kiuchumi.

"Kwanza nimeoneshwa ofisi ya uhamiaji katika stesheni ya Dar es Salaam nikajiuliza ni ya nini, mwisho nikapata kufahamu kumbe SGR ni mradi wa Kimataifa, nimefurahishwa sana na ujenzi huu" Amesema Bi Mariane Diop.

Wajumbe wengi katika ziara hii wameeleza kufurahishwa kwao na ujenzi huu mkubwa wa mradi wa SGR na wameziomba nchi za Afrika kufanya uwekezaji wa namna hii katika kuleta maendeleo chanya Afrika.