Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WASHIRIKI KOZI FUPI YA UTEKELEZAJI WA SERA NA MIPANGO WATEMBELEA SGR


news title here
14
February
2023

WASHIRIKI KOZI FUPI YA UTEKELEZAJI WA SERA NA MIPANGO WATEMBELEA SGR

Washiriki wa kozi fupi ya utekelezaji wa sera na mipango kwa viongozi kutoka chuo cha Taifa cha Ulinzi wametembelea Shirika la Reli Tanzania – TRC kuona maendeleo ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha kwanza Dar es Salaam – Morogoro, Februari 2023.

Mkuu wa chuo cha Taifa na Ulinzi Meja Jenerali Ibrahimu Mhona amesema lengo la kutembelea TRC ni kuwapa fursa washiriki wa kozi wakiwemo wakuu wa wilaya, wakurugenzi na makatibu tawala wa wilaya mbalimbali nchini Tanzania kujua TRC inavyofanya kazi sambamba na kauli mbiu ya “Uongozi wa kimkakati kwa mazingira yanayobadilika kiusalama Tanzania”.

Meja Jenerali Mhona ameipongeza TRC kwa kuweza kusimamia ujenzi wa miundombinu, kupitia ziara hii washiriki wamejifunza na kuona uendeshaji wa Shirika unavyofanyika pamoja na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya TRC na bandari katika usafirishaji.

“Kupitia ziara hii tumejifunza ujenzi wa SGR kuwa ni fursa kwa watanzania sababu itawezesha kusafirisha bidhaa zao kwa muda mchache pamoja na abiria watasafiri kwa muda mfupi kwahiyo hii itaokoa muda na kumuwezesha mtu kufanya mambo mengine, pia nawaambia mabehewa ya SGR ni mazuri na yamezingatia ubora na usalama wa usafiri kwa abiria” amesema Meja Mhona.

Mkurugenzi Mkuu TRC Masanja Kadogosa amekishukuru chuo cha Taifa cha Ulinzi kwa kutembelea TRC kwaajili ya washiriki wa kozi fupi kuona maendeleo ya mradi wa kimkakati wa reli ya kisasa kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali katika mradi.

“Reli yetu ni njia mtambuka inayounganisha bandari ili kusafirisha mizigo, kwahiyo ziara hii itasaidia kuendelea kuitangaza reli yetu ndani na nje ya nchi ili tuweze kuvutia biashara ya usafirishaji kwa kutumia reli nchini” alisema Kadogosa.

Mmoja wa washiriki wa kozi fupi Mkuu wa Wilaya ya Rorya Juma Chikoka amesema mradi wa SGR ni mradi utakaokidhi matakwa ya watanzania na umezingatia ubora vilevile utatatua changamoto ya usafiri nchini pamoja na kuunganisha nchi jirani ikiwemo Demokrasia ya Congo na Tanzania itakua kitovu cha usafirishaji na uchumi kupitia mradi huu wa reli ya kisasa.

“Mradi huu umeweza kutoa ajira kwa wazawa katika vipande vyote vya ujenzi vinavyoendelea kujengwa hadi sasa kwahiyo watanzania tunatakiwa tujivunie mradi huu na kupitia mradi huu tunaona dira ya Tanzania wapi tulipotoka na wapi tunapoenda” amesema Juma Chikoka.