Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WASHINDI WA UANDISHI WA INSHA WATEMBELEA MRADI WA SGR DAR ES SALAAM – MOROGORO


news title here
09
April
2021

Washindi wa Shindano la uandishi wa Insha za Masoko lililoandaliwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) watembelea Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro Aprili 09, 2021.
Washiriki hao ambao ni wanafunzi wa Vyuo Vikuu tofauti hapa nchini wameongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA Bwana Nicodemus Mkama kutembelea mradi wa SGR kwa lengo la kuona faida za mradi na kujifunza namna shughuli za Masoko na Biashara zinavyoweza kuleta fursa ya kukuza mitaji na dhamana kupitia miundombinu ya reli inayojengwa hivi sasa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Bwana Nicodemus Mkama ameeleza kuwa ziara hiyo imekuwa muhimu kwa taasisi yao kwakuwa wamepata fursa ya kutembelea mradi huo wa kimkakati ambapo waliweza kuona Stesheni ya Dar es Salaam, Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere na Morogoro sambamba na miundombinu mingine ikiwemo ya umeme.
“Hii inaonesha ni kwa jinsi gani fedha zinazokusanywa kupitia masoko na mitaji zinaweza kusaidia katika kuleta faida na fursa kwa watanzania, natoa shukurani kwa uongozi wa Shirika la Reli kwa kutupa fursa hii” alisema Ndugu Nicodemus
Bwana Nicodemus aliongeza kuwa wameongozana na Washindi ambao wamepata tuzo kutoka CMSA ili waweze kujifunza kwa vitendo jinsi gani Miradi hii inaweza kuleta fursa na faida kupitia Masoko na Mitaji ambapo Ndugu Nicodemus alieleza kwa kutolea mifano kwa baadhi ya makampuni yaliyofaidika moja kwa moja na mradi wa SGR,
“Twiga Cement na Tanga Cement ni moja kati ya makampuni yaliyopata Mitaji kutoka katika Soko la Mitaji ambapo yameweza kuuza malighafi katika Mradi huu wa SGR” aliongeza Bwana Nicodemus
Mmoja kati ya Wanafunzi walioshiriki ziara hiyo, Jackline Nicodemus Mushi alisema kuwa “Nimejifunza kuhusu mambo mengi ikiwemo kutofautisha SGR na MGR, pia tumeona mradi wa SGR kuwa ni mkubwa na mzuri ambapo katika maeneo ya Stesheni ujenzi wake umeweka mazingira mazuri ya kibiashara”
Naye Rodgers Rujagusa, mshindi wa shindano la uandishi wa Insha za Masoko alieleza kuwa, “Nimejifunza vitu vingi, ikiwemo umuhimu wa kulipa Kodi ambapo zinakwenda kutekeleza miradi ya namna hii yenye kuleta maendeleo ya nchi pamoja na kuunganisha nchi jirani ambazo hazina bandari ikiwemo Rwanda, Congo na Burundi”
Naye Mhandisi Simon Mbaga, Meneja Mradi wa SGR Dar es Salaam – Morogoro ameeleza kuwa ziara ya CMSA ni muhimu kwa sababu ni wadau wakubwa katika kuchangia Mapato kupitia mifumo ya fedha ya serikali, aliongeza kuwa wageni wamefurahi, wameona kazi na wameshuhudia fedha zao zinavyotumika.