Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WASANII, MASHABIKI WA SIMBA NA YANGA WAFIKA MKOANI KIGOMA


news title here
24
July
2021

Mashabiki wa mpira wa miguu wa Simba na Yanga pamoja na Wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya waingia mkoani Kigoma leo Julai 24, 2021 kwa kutumia usafiri wa treni ya Deluxe wakitokea Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na Tabora, kwa ajili ya kushuhudia mechi kati ya Simba na Yanga inayotarajiwa kuchezwa Julai 25, 2021.

Safari hiyo ambayo imeongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ambaye ameeleza kuwa mashabiki wamefurahia usafiri wa treni kutokana na burudani mbalimbali ndani ya treni ikiwemo muziki pamoja na michezo ikiwemo drafti, michezo ya televisheni pamoja na bao.

Aidha, Ndugu Kadogosa amesema kuwa treni hiyo itaanza safari ya kurudi Dar es Salaam majira ya saa tatu usiku mara baada ya mechi itakapomalizika, hivyo amewasisitiza abiria waliokata tiketi za kwenda na kurudi na wale wanaohitaji usafiri wa treni kufuata taratibu mapema ikiwemo kukata tiketi na kuwahi stesheni ili kuepusha usumbufu.

Pia Ndugu Kadogosa amewataka wananchi wa mkoa wa Kigoma kukaa tayari kwa ajili ya kupokea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGRambao upo kwenye mpango wa serikali, reli hiyo itaunganishwa kutoka Tabora hadi Kigoma ambayo itapunguza muda wa safari hadi saa nane kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma.

“Watu wa Kigoma wanapaswa kuchangamkia fursa, kuna fursa nyingi zinakuja kwa ajili ya kukuza miundombinu ya usafiri wa treni” alisema Ndugu Kadogosa.

Hata hivyo Ndugu Kadogosa amewaeleza wananchi uzuri wa usafiri wa treni ambao pia ni utalii kwa abiria kuona sehemu mbalimbali pamoja vivutio vya nchi .

“Tumesafiri takribani Kilometa 1300, watu wameona vitu vingi ambavyo hawajawahi kuviona kama mto Malagarasi, Ziwa Tanganyika, wameona ujenzi wa mahandaki Kilosa” alisema Ndugu Kadogosa.

Msanii wa muziki wa kizazi kipya Lulu Hassan maarufu kama Lulu Diva ni mmoja kati ya wasanii waliosafiri na treni ya Deluxe, amefurahishwa na Safari na kuongeza kuwa ni mara yake ya kwanza kupanda treni kwenda Kigoma hivyo amejifunza vitu vingi kwa kutumia usafiri wa treni pamoja na kuona vivutio tofauti vya nchi.

“Kiukweli sijaamini kama nimefika Kigoma kwa haraka kiasi hiki “ alisema Lulu Diva.