Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WANAWAKE WA TRC WASHEREHEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI


news title here
08
March
2023

Wanawake wa Shirika la Reli Tanzania waungana na wanawake wengine kote nchini kusherehekea sikukuu ya wanawake Duniani iliyoadhimishwa kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar ss Salaam, Machi 08, 2023.

Siku ya wanawake mwaka 2023 imebeba kauli mbiu isemayo “Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia ni chachu katika kuleta Usawa wa Kijinsia” imewataka wanawake wafanye kazi kwa bidii na ubunifu wa hali ya juu unaoendana na mabadiliko ya kiteknolojia ili kuleta maendeleo na usawa katika jamii ya Tanzania na Dunia.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu TRC Bi. Amina Lumuli amewataka wanawake wa Shirika la Reli watumie nafasi walizonazo kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kujenga Shirika na kuleta maendeleo katika nchi na ustawi wa jamii kwa ujumla.

“Tunaposherehekea sikukuu ya wanawake na kusema kauli mbiu ya Ubunifu na mabadiliko ya Teknolojia ni chachu katika kuleta usawa wa kijinsia, kila mmoja kwa nafasi yake atafakari haya mabadiliko yeye anaendana nayo vipi, mabadiliko yanakuja kwa kasi sana, tuna Rais mwanamke nadhani anatutia moyo, kila mmoja wetu anatamani afike mbali kama yeye”. amesema Bi. Amina.

Aidha, Bi. Amina Lumuli ameongeza kuwa Dunia imekuwa kijiji kimoja kutokana na maendeleo na ukuaji wa teknolojia hivyo amewataka wanawake wa TRC kuwa wabunifu kwenye utendaji ili waweze kuongeza kipato na kuzisaidia familia, jamii na nchi kwa ujumla.

“Tunahitaji ubunifu zaidi, ukiangalia hata majumbani mwetu mfano wanawake tunaweka vibubu, baba akikwama mama unafungua kibubu unaongezea kwenye bajeti, kwahiyo kwa ubunifu wetu tunaweza tukasaidia majirani, watoto yatima, ndugu na familia kwa ujumla”. amesema Mkurugenzi.

Naye Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji kutoka Shirika la Reli Tanzania Bi. Nzeyimana Dyegula amesema kuwa siku ya wanawake Duniani imeweza kutambua mchango na nafasi ya wanawake kwenye jamii katika kutimiza majukumu mbalimbali ambayo yanachochea maendeleo ya kiuchumi kwenye nchi na Dunia.

“Kwa sasa TRC kuna mabadiliko makubwa sana, ujenzi wa reli ya kisasa umekuja na mabadiliko ya teknolojia ambayo yameruhusu wanawake wengi zaidi kuajiriwa tofauti na hapo awali ambapo reli ya zamani (MGR) ilihitaji uendeshaji kwa kutumia nguvu zaidi na wanaume wengi walifanya kazi kwenye reli hiyo ya zamani tofauti na sasa ambapo reli ya SGR inahitaji ubunifu na utumiaji wa teknolojia katika uendeshaji”. amesema Bi. Nzeyimana.

Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka Machi 08, ikiwa ni harakati za kutambua mchango na ushirikishwaji wa wanawake kwenye kupambania haki na kuleta usawa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.