Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC YAANZA KUUNDA VICHWA VYA TRENI ZA MGR NCHINI


news title here
14
March
2026

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu, imelitolea wito Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendelea kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania wanaounda na kukarabati vichwa vya treni za MGR, kwa kuwapa mafunzo thabiti ndani na nje ya nchi ili kuongeza maarifa, stadi na ubunifu katika utendaji wao kazi hiyo .

Wito huo umetolewa Machi 14, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso, wakati wa ziara ya kamati hiyo iliyolenga kukagua mradi wa uundaji wa vichwa vya treni za MGR, unaoendelea katika karakana ya Pugu, Jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Kakoso kwa niaba ya kamati hiyo, ameitaka TRC kuhakikisha inawapa fursa na kuwapeleka vijana hao wenye ujuzi nje ya nchi kujifunza na kuchota utalaamu zaidi ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao, aidha alitoa rai kwa TRC kuwapa k kipaumbele katika suala la ajira ili waendelee kulitumikia shirika na nchi kwa uaminifu.

Aidha Mhe. Kakoso, alisema kamati inaipongeza kwa dhati TRC na Mkurugenzi wake Mkuu Mhandisi Machibya Shiwa, ambapo kwa mara ya kwanza katika historia, Tanzania imefanikiwa kufanya hivyo kufuatia ucheleweshwaji wa vipuri kimkataba kutoka kwa wazabuni wa vipuri wa SMH Kutokana vita kati ya Ukraine na Urusi, hivyo TRC ilifanya maamuzi ya kusafirisha vichwa viwili vilivyokamilika na kuundwa nchini Malaysia na kusafirisha vipuri kutoka kw wazabuni kuja nchini na kuanzaz uundwaji wa vichwa sita vilivyobaki katika karakana ya Pugu.

Mhe. Kakoso, ameongeza kusema kuwa uamuzi wa TRC kuunda vichwa vya treni hapa nchini umepunguza gharama kubwa ambayo serikali ingetumia kuagiza vichwa hivyo na pia imewezesha vijana wengi wa Kitanzania wenye ujuzi kuajiriwa aidha Mhe. Kakoso amewaasa watumishi wa Shirika la Reli Tanzania kuwa wazalendo katika kulitumikia Shirika na kutunza rasilimali zilizopo na kuepuka vitendo vya hujuma kwa shirika.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi Mhe.David Kihenzile, ameendelea kuipongeza Serikali kupitia TRC kwa kukuza sekta ya uchukuzi kwa kuendelea kujenga miundombinu bora na yenye ufanisi na kununua vitendea kazi ikiwemo vichwa na behewa.

"Nampongeza rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya uchukuzi , serikali imeendelea na ujenzi wa reli ya kisasa zaidi ya kilomita 2290 na sasa inanunua vitendea ili kuboresha sekta hii." alikazia Mhe.Kihenzile.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Mhandisi Machibya Shiwa, Pamoja na masuala mengine, aliiambia kamati hiyo ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu juu ya manufaa ya mradi wa uundaji wa vichwa vya treni za MGR Daraja la 91XX katika karakana ya Pugu, ni Pamoja na fursa za ajira amabpo jumla ya vijana 34 ambao hawakuwa wameajiriwa sasa wameajiriwa kupitia mradi huo. Aidha Mhandisi Shiwa, alisema, “kupitia mradi huo baadhi ya Watanzania, wamepata kuuza bidhaa zinazotumika katika uundaji wa vichwa hivyo nao ni kama wenye mashine za kuchinga vipuri, wauzaji wa vifaa ujenzi, bolt na nati, wauzaji vifaa vya umeme, mabomba, wauzaji vilainishi, bidhaa za mpira nk’’, alimalizia Mkurugenzi mkuu huyo wa TRC.

------------mwisho-------------------