Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANAWAKE TRC WASHEREHEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI


news title here
08
March
2022

Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania - TRC Ndugu Masanja Kadogosa amejumuika pamoja na wanawake wa TRC kusherehekea siku ya wanawake Duniani katika jengo la Stesheni ya reli ya kisasa – SGR jijini Dar es Salaam, March 8 2022.

Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka ikiambatana na kauli mbiu ambayo huleta hamasa kuwapa nguvu Wanawake katika kutimiza majukumu yao ya kila siku na kuchangia katika kuleta maendeleo. Kauli mbiu ya Siku ya Wanawake kwa mwaka 2022 ni ”Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu: Tujitokeze kuhesabiwa”.

Shirika la Reli Tanzania lina wafanyakazi wengi wanawake katika kada mbalimbali ikiwemo Wakurugenzi na wakuu wa Vitengo, wahandisi, madereva wa treni, mafundi, wahasibu, waongoza treni, wakaguzi wa reli, wakuu wa vituo pamoja na nafasi nyingine mbalimbali ndani ya shirika.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkurugenzi Mkuu TRC Masanja Kadogosa amesema kuwa ongezeko la idadi ya viongozi wanawake, watendaji na wafanyabiashara ni faraja katika kuleta maendeleo ya nchi.

“Leo hii tunasherekea siku ya wanawake Duniani kipekee zaidi tukiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwanamke na tukiwa na idadi kubwa ya viongozi wanawake, wafanyabiashara pamoja na wachapakazi wengi zaidi wa kike” alisema Kadogosa.

Bi. Lucy Kigondi kutoka Idara ya Usafirishaji amesema kuwa wanawake TRC wanafanya kazi kwa bidii kama ikiwemo yeye husimamia kanda zote tatu za TRC katika idara ya usafirishaji zikiwemo kanda ya Dar es Salaam, kanda ya Tanga pamoja na kanda ya Tabora.

“Kwa sasa wanawake tunafanya kazi kama wanaume wanavyofanya, mfano idara ya usafirishaji tunafanya kazi kwa zamu wanawake tuna zamu za usiku kama wanaume na vilevile tupo katika nafasi za uongozi wa vituo, uongozaji treni tupo na wanaume pia” alisema Bi. Lucy

Naye Katibu Muhtasi Bi. Prisca Ndaigeze amesema wanawake TRC wamejipanga kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha TRC inafikia malengo na wataendelea kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja wote wakiwemo abiria na wasafirishaji mizigo.

“Sisi wanawake wa TRC Pamoja na Tanzania nzima tutaiishi kauli mbiu ya kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu tujitokeze kuhesabiwa vile vile amewaasa mabinti kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia vipato vyao kwa njia iliyo halali” alisema Bi. Prisca.

Bi. Aisha Mapondela, ‘Stock Controller’ idara ya usafirishaji Kanda ya Dar es Salaam amesema idadi ya wanawake katika idara ya usafirishaji imeongezeka.

“Kazi yangu ni kufuatilia treni zote kutoka Dar es Salaam, Ilala, Malindi hadi Dodoma ambako ndio mwisho wa kanda ya Dar es Salaam na kuelekea Tanga kanda ya Dar es Salaam huishia Wami na kazi hii hufanyika kwa kushirikiana na kiongozi wa kituo husika” Bi. Aisha.