WANANCHI ZAIDI YA ELFU MOJA NA MIA TATU WAMEPOKEA HUNDI KATIKA ZOEZI LA FIDIA IHUMWA - DODOMA

May
2020
Wananchi zaidi ya 1,300 wamepokea hundi katika zoezi la malipo ya fidia Ihumwa jijini Dodoma , ikiwa ni zoezi endelevu linalofanyika katika mtaa wa Ihumwa ili kuhakikisha wananchi wote waliopitiwa na mradi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha Morogoro - Makutupora waweze kupisha ujenzi wa reli ya kisasa uendelee katika eneo hilo, hivi karibuni Mei, 2020.
Shirika la Reli Tanzania - TRC limeendeleza zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi wa mtaa wa Ihumwa na kuhakikisha awamu zote za ulipaji wa fidia katika mtaa huo zinaenda kwa wakati ikiwa hivi sasa ni awamu ya tatu ya ulipaji huo .
Takriban wananchi zaidi ya elfu mbili wanaotakiwa kulipwa fidia katika mtaa wa Ihumwa jijini Dodoma ambapo zoezi hilo limeshakamilika katika awamu ya kwanza na ya pili na hivi sasa kuendelea na awamu ya tatu ya ulipaji wa fidia.
Muhasibu kutoka TRC Bw. Nicholaus Majumbi amesema kuwa hadi sasa hali ni shwari na wananchi wanaendelea kujitokeza kwa wingi kadri ya idadi ya watu wananopangiwa kuchukua hundi zao kwa siku kwa lengo la kuepusha mikusanyiko isiyo ya lazima katika janga hili la virusi vya Corona.
“Tumepanga watu wachache ili kuzuia msongamano katika kipindi hiki kigumu“ alisema Bw. Nicholaus.
Mwenyekiti wa mtaa wa Ihumwa Bw.William Josia Njilimuyi ameishukuru sana Serikali ya awamu ya tano kupitia Shirika la Reli kwa kuhakikisha wananchi wa mtaa huo wanapatiwa fidia zao ili kuepusha migogoro baina ya wananchi na Serikali.
Pia ameipongeza TRC kwa kufuata maelekezo ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya corona katika ufanyaji wa zoezi la malipo kwa kuhakikisha kila mwananchi ananawa mikono kwa maji na sabuni na watumishi kuvaa barakoa pamoja na kutumia kitakasa mikono (Sanitizer).
“wananchi wamefurahi na wanaendelea kusubiri awamu nyingine ya malipo“ alisema Bw. Njilimuyi.
Mtaa wa Ihumwa ni moja kati ya mitaa ambayo wananchi wengi wamepitiwa na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa. TRC inaendelea kutoa shukurani kwa wananchi watanzania kwa ushirikiano mzuri kufanikisha zoezi hili, na kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais Dr. John Pombe Magufuli katika kuimarisha miundombinu ya reli nchini.