Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WILAYANI MANYONI WAFAIDIKA NA FIDIA


news title here
05
October
2023

Zoezi la ulipaji fidia linalofanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) linaendelea kufanyika kwa wananchi na wengi waliopisha ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa wanajitokeza kupokea malipo katika kipande cha tatu kwenye mradi wa SGR Makutupora - Tabora, Shirika la Reli Tanzania linafanya malipo katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida Octoba 2023.

Takribani Hundi 319 zimelipwa na zingine zinaendelea kulipwa, wananchi wanalipwa baada ya kupisha maeneo yao kwaajili ya ujenzi wa njia kuu ya reli SGR katika kipande cha tatu Makutupora - Tabora.

Afisa Miliki kutoka TRC Bw. Aristides Rwebangira amesema zoezi la ulipaji fidia linafanyika katika wilaya ya Manyoni katika vitongoji vinne mjini Manyoni, hadi sasa fidia imelipwa katika vitongoji vya Majengo, Tambukareli na Chang'ombe na zoezi linaendelea katika kitongoji cha Kipondoda pia litafanyika kata ya Muhalala katika kitongoji cha Gengeni na Kijiji cha Sukamahela katika kitongoji cha Chiwondo wilayani Manyoni mkoani Singida.

"Tunaomba wananchi waendelee kufika kwa wakati katika ofisi za serikali za Mitaa ambako timu ya TRC ipo kwaajili ya malipo ya fidia kwa wananchi, wafike na nyaraka zote muhimu zinazowezesha malipo kufanyika" ameongeza Rwebangira.

Mthamini kutoka Wizara ya Ardhi Bw. Iddi Muhibu amesema wananchi wanalipwa hundi za malipo kulingana na uthamini ulivyofanyika kwa kufuata taratibu na Sheria za uthamini wa Ardhi.

"Tunafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na timu kutoka TRC pamoja na viongozi wa serikali za mitaa kwahiyo zoezi hili linafanyika vizuri na Kila mwananchi anapata stahiki yake kwa malipo halali". amesisitiza Muhibu.

Mtendaji wa Kata ya Manyoni Mjini Bw. Ewani Watsoni Simkonda ameishukuru serikali na TRC kwa kuwezesha malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa njia ya reli katika kipande cha tatu Makutupora - Tabora.

Shirika la Reli Tanzania linaendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wote waliotwaliwa maeneo yao kupisha ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa katika sehemu zote ambako SGR imepita.