Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WILAYA YA MASWA - SIMIYU WAJIVUNIA MRADI WA SGR


news title here
29
May
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la kutwaa ardhi katika kijiji cha Mwabagalu na Nyabubinza wilayani Maswa mkoa wa Simiyu kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha tano Isaka - Mwanza hivi karibuni Mei, 2022.

Zoezi hilo la utwaaji wa ardhi katika maeneo ya makaburi ambayo yamepitiwa na mradi huo wa SGR linasimamiwa na uongozi kutoka TRC, viongozi wa kijiji, afisa afya wa wilaya, afisa ardhi pamoja na afisa tarafa.

Mhandisi kutoka TRC Bw. Blasius Mwita amesema kuwa wananchi wanajitokeza kwa wingi kutoa ushirikiano katika zoezi pamoja na kufuata taratibu zote zinazohitajika ili kuwa na usalama kwa watendaji pamoja na wananchi.

“Tunahakikisha tunasimamia vyema zoezi hili kiusalama na kiafya ili kuepusha milipuko ya magonjwa “ alisema Mhandisi Mwita.

Aidha, Mhandisi Mwita alieleza kuwa kupitia mradi huo wananchi watapata fursa mbalimbali kibiashara hasa katika mifugo kwa kuweza kusafirisha kutoka mikoa ya kanda ya ziwa hadi Dar es Salaam kwa mud mfupi.

“Huu mradi ni wakwetu sote, wafugaji watapeleka nyama na kuuza wenyewe, hali ya wanakijiji itabadilika na biashara itazidi kutanuka“ alisema Mhandisi Mwita.

Naye Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Bw. Peter Nestory ameeleza kuwa wananchi wanaendelea kuwa na uelewa katika masuala ya afya pia wanaendelea kutoa elimu hasa katika mazoezi hayo ili kuweza kujiepusha kuendelea kukaribia maeneo ambayo miili imetolewa kuepukana na matatizo mbalimbali yatakayoweza kujitokeza.

“Tunahakikisha tunamwagia dawa kali ili kuua vijidudu vitakavyoleta milipuko ya magonjwa“ alisema Bw. Peter.

Vilevile Bw. Peter alisema kuwa vibarua wote wa kufukua wanapatiwa nyenzo za kufanyia kazi kiusalama kama vile barakoa, mavazi, buti, gloves pamoja na kunawa na dawa baada ya kazi.

Mwananchi kutoka katika kijiji cha Nyabubinza Bw. Salinja Ligwa amesema kuwa mradi wa SGR ni mradi mkubwa utakaoweza kubadilisha maisha ya wanakijiji kuwa na kilimo cha kisasa na ufugaji ili kuweza kukuza biashara na vijiji kuchangamka kwa kuleta wawekezaji wakubwa katika maeneo mbalimbali.

Mradi huo wa SGR unaendelea kuleta manufaa katika mikoa mbalimbali kwa wananchi kupata fursa za ajira katika mradi pamoja na biashara kuzidi kutanuka vijijini na mijini