WANANCHI WALIOPISHA UJENZI WA SGR MWANZA – ISAKA WAENDELEA KULIPWA STAHIKI ZAO

August
2022
Zoezi la malipo ya fidia kupisha mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR linaendelea kufanyika kwa wananchi wa mkoa wa Mwanza na Shinyanga ambao maeneo yao yametwaliwa na Shirika la Reli Tanzania - TRC kwa lengo la kupisha ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR, kipande cha tano (5) Mwanza – Isaka, Agosti 2022.
Jumla ya hundi za malipo 573 zilizoandaliwa na Shirika la Reli zinaendelea kulipwa kwa wananchi katika vijiji 24 vya mkoa Mwanza na Shinyanga. Akizunguza na wananchi wa kijiji cha Didia, Shinyanga Mhandisi Oliva Julius kutoka TRC alitoa wito kwa wananchi na viongozi wa vijiji kutoa ushirikano wa kutosha ili kuhakikisha walengwa wa malipo ya fidia wanapatikana ili kuhakikisha wanalipwa stahiki zao na mkandarasi kuendelea na ujenzi wa reli ya kisasa.
Kutokana na changamoto mbalimbali za uelewa kwa wananchi kuhusu namna Wizara ya Ardhi inavyozingatia uthamini wa ardhi, majengo na mazao na kuhakikisha wanapewa fidia stahiki, Maafisa kutoka Shirika la Reli na viongozi wa vijiji walianza kwa kutoa elimu kabla ya zoezi kuanza kuwaelezea wananchi namna mchakato wa uthamini ardhi na mali zote unavyofanyika na hatimaye kuwapa kile kinachostahili kulingana na Sheria ya ardhi inavyosema.
Hata hivyo wananchi wameendelea kuishukuru Serikali kwa kujali na kuthamini utayari wao wa kuachia maeneo waliyokuwa wanamiliki kwaajili ya kupisha maendeleo ya watanzania wote, kwa upande mwingine wamewapongeza maafisa wa TRC kwa elimu waliyoitoa ambayo imepelekea wao kupokea malipo hayo wakiwa hawana wasiwasi kama ilivyokuwa kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha wa uthamini wa ardhi.
Wenyeviti wa vijiji waliwataka wananchi endapo watapokea malipo haya yakawe chachu katika kukuza uchumi wao na kubadilisha mfumo mzima wa maisha kwa kujenga nyumba bora, kusomesha watoto pamoja na kuanzisha biashara.