Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WAJIVUNIA MRADI WA SGR MWANZA - ISAKA


news title here
01
December
2021

Shirika la Reli Tanzania- TRC linaendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha tano Mwanza - Isaka ambapo wananchi wameonesha kujivunia uwepo wa mradi wa SGR kufuatia kupata stahiki zao kwa wakati katika zoezi hilo la ulipaji fidia lililofanyika katika maeneo mbalimbali mkoani Mwanza, Simiyu na Shinyanga hivi karibuni Novemba, 2021.

Zoezi hilo ambalo linasimamiwa na maafisa kutoka TRC, maafisa ardhi wa wilaya husika, wathamini pamoja na viongozi wa kijiji ambao wanahakikisha zoezi linaenda kwa wakati na kwa kuhakikisha kila mstahiki anakabidhiwa hundi kulingana na thamani wa mali zake.

Afisa ardhi kutoka TRC Bw. Ramadhan Mfikilwa amesema kuwa zoezi linaenda vyema katika maeneo yote ambayo wananchi wanakabidhiwa hundi zao kwa kufuata taratibu zote wanazofahamishwa na uongozi wa kijiji husika.

“Mwananchi anatakiwa kuja na nyaraka za uthamini wa eneo, nakala ya kitambulisho cha kura ama cha taifa na barua ya utambulisho kutoka kwa mtendaji wake” alisema Bw. Ramadhan.

Pia Bw. Ramadhan alisema kuwa timu ya TRC ikishirikiana na viongozi wa kijiji inahakikisha inatoa taarifa mapema kwa wananchi ili kuweza kujiandaa na zoezi kuepusha usumbufu wowote utakaojitokeza.

“Tunaendelea na zoezi na hadi sasa tumegawa hundi kwenye vijijini kumi “ alieleza Bw. Ramadhan.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mwagala wilayani Misungwi Bw. Raphael Matalu amesema kuwa wananchi wa kijiji hicho wamefurahishwa na mradi wa SGR kupita katika maeneo yao kwa kuwa watajikwamua kimaendeleo hasa vijana wao kupata ajira ndani ya mradi na pia biashara kuongezeka kwa wingi.

“Wananchi wanajivunia kupita kwa mradi huu kwa kuwa utarahisisha usafiri kwa kiasi kikubwa” alizungumza Bw. Matalu.

Vilevile mwananchi wa kijiji cha Mwagala wilaya ya Misungwi, Mwanza Bi. Shinje Gamba ameeleza kuwa malipo hayo ya fidia aliyoyapata yatamsaidia kujenga nyumba ya tofali na kusomesha watoto wake.

“Serikali imenikomboa sana, sina budi kuishukuru na Mungu afanye mradi huu kuwa wa kimataifa” alisema Bi. Shinje.