Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WAENDELEA KUUNGA MKONO UJENZI WA MRADI WA SGR


news title here
19
November
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea kufanya zoezi la utwaaji ardhi kwa wananchi ili kupisha ujenzi wa njia ya umeme katika ujenzi mradi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha pili Morogoro - Makutupora linalofanyika mkoani Dodoma hivi karibuni Novemba, 2022.

Maeneo yaliyotwaliwa ni pamoja na mtaa wa Zuzu, Soweto, Ntyuka, Miganga, Iyumbu na Chololo yaliyopo Manisipaa ya Dodoma Jiji kwaajili ya zoezi la uhamishaji wa makaburi takribani 50.

Afisa maswala ya jamii kutoka TRC Bw. Leodgard Otaru amewaeleza wananchi kuwa ulipaji wa kifuta machozi kwa wasimamizi husika utafuata baada ya kukamilisha zoezi la kuwahamisha wapendwa wao na kuwapumzisha katika eneo husika lililopangwa na serikali ya mtaa.

“Tunawafahamisha wananchi juu ya taratibu zote za ulipaji kifuta machozi kwamba zimeainishwa na ofisi ya hazina na fedha zitalipwa baada ya zoezi ili kujiridhisha na idadi kamili ya miili iliyopatikana” alisema Bw. Otaru.

Pia Mthamini kutoka Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali Bw. Mathayo Mitole alisema kuwa uthamini wa mali ikiwemo thamani ya jengo, mashamba, mazao na ardhi unafanyika kwa weledi na ufanisi kwa kufuata kanuni na taratibu za kufanya uthamini ili kuepusha migogoro na malalamiko kutoka kwa wananchi.

“Katika kufanya uthamini tunafuata sheria ya uthamini na utajiri wa wathamini ya mwaka 2016 ( Evaluation and Valuers Registration Act ) hii inayotoa miongozo mbalimbali ya uthamini wa mali na pia sheria ya uthamini inayotoa miongozo ya fidia na kanuni zake ( Land Acquisition Act ) ya mwaka 1967” alisema Bw. Mitole.

Naye Bw. Hindi Sukwe mkazi wa mtaa wa Miganga amefurahishwa na maendeleo ya mradi wa SGR kwa kuwa chachu ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ambapo uendeshaji wa treni ya kisasa utamuwezesha mwananchi kusafiri na kuweza kusafirisha mizigo.

“Tunahitaji kulima na kuuza mazao yetu sehemu zenye masoko makubwa hivyo SGR hakika itakua mkombozi wetu “alisema Bw. Sukwe.

Mradi wa SGR unaendelea kuleta hamasa ya maendeleo kwa wananchi hivyo utaleta mapinduzi katika kukuza sekta ya usafirishaji kwa kutumia reli pamoja na kuongeza pato la taifa.