Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WAENDELEA KUTOA MAENEO KUPISHA NJIA YA UMEME MRADI WA SGR


news title here
03
November
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la utwaaji ardhi ili kupisha njia ya umeme ya ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa - SGR kipande cha pili Morogoro - Makutupora lililofanyika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro hivi karibuni Oktoba, 2022.

Zoezi hilo la utwaaji ardhi linaambatanisha uhamishaji wa makaburi ambapo takribani makaburi 80 yamehamishwa katika maeneo mbalimbali.

Mhandisi kutoka TRC Bw. Juma Kadashi alisema kuwa tathmini ya maeneo hayo ilifanyika vyema hivyo zoezi hilo la uhamishaji makaburi linaenda sambamba na zoezi la ulipaji fidia kwa ndugu waliopoteza wapendwa wao.

Pia Mhandisi Kadashi alieleza kuwa serikali za vijiji zimetenga maeneo maalumu kwaajili ya kuwapumzisha wapendwa wao na vilevile inaendelea kuwasihi wananchi kwenda kuzikia sehemu hizo zilizotengwa ili kuleta maendeleo ya mipango miji katika maeneo yao.

“Njia ya umeme itapeleka umeme katika stesheni za umeme za SGR kitaalamu zinaitwa TPS (Traction Power Substation) ambazo zitapokea umeme mkubwa wa takribani Kilovoti 220 (220kv) na umbali wa TPS moja mpaka nyingine ni kilomita 50” alisema Mhandisi Kadashi.

Aidha Mhandisi Kadashi alisema kuwa wananchi pamoja na viongozi wa vijiji wanaendelea kutoa ushirikiano na kuhakikisha zoezi linakwenda kwa kufuata taratibu zote ambazo zimeandaliwa na timu kutoka TRC.

Naye Kaimu Mkuu kutoka Kitengo cha Usafi na Mazingira kutoka wilayani Kilosa Anthony Mbise alisema kuwa ushirikishwaji wa wataalamu wa afya kwenye zoezi hilo ni muhimu katika kuhakikisha jamii inakua salama ili kuzuia magonjwa ya milipuko katika maeneo hayo.

“Zoezi linafuata taratibu zote za kiafya katika kujikinga na bakteria, virusi pamoja na fangasi wanaokaa kwa muda mrefu hawa wanaweza sababisha magonjwa kwa njia ya hewa na hata kusambaa hivyo tunawadhibiti na kuwamwagia madawa kabla mwili haujatolewa” alisema Bw. Mbise.

Pia Mkazi wa kijiji cha Munisagara Bw. Koroneli Malisali alisema kuwa tangu mradi huo wa SGR uanze umeleta maendeleo vijijini kwa wananchi kusafirisha mazao yao kiurahisi , kuwa na nyumba za kisasa kupitia fidia wanazopatiwa pamoja na huduma za kujamii kuongezeka kwa wingi.

“Kiukweli tunamshkuru sana Mungu tangu kijiji hiki cha Munisagara kipate hati ya kuwa kijiji mwaka 1973 hatukuwai kuona barabara inapita hapa ila sasa mradi wa SGR umetuletea maendeleo vijijini “ alisema Bw. Koroneli.

Mradi wa SGR unaendelea kuleta matokeo chanya katika maeneo mbalimbali ya vijiji pamoja na miji kwa kuleta sura mpya ya kimaendeleo nchini.