Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WAENDELEA KUPOKEA STAHIKI ZAO KUPISHA MRADI WA SGR


news title here
05
August
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliotwaliwa maeneo kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha pili Morogoro - Makutupora kwenye maeneo mbalimbali ya Dodoma, Bahi na Manyoni Agosti, 2023.

Zoezi hilo la fidia limegusa maeneo kwaajili ya uchimbaji vifusi, njia za juu na njia za chini, maeneo ya kumwaga udongo usiofaa kwa ujenzi kwenye ujenzi wa SGR.

Afisa Ardhi kutoka TRC Bi. Tereza Nyatega alisema kuwa TRC inaendelea kutwaa ardhi kwa wananchi katika maeneo ambayo yana uhitaji kwa mkandarasi na kufanya malipo kwa wananchi wote wanaostahili kupatiwa fidia ama kifuta machozi kwa upande wa makaburi.

“Maeneo huongezeka kulingana na uhitaji wa mkandarasi sababu ujenzi wa SGR ni kusanifu na kujenga hivyo eneo likihitajika linafanyiwa uthamini na baadaye wananchi wanapatiwa stahiki zao” alisema Bi. Tereza.

Mthamini kutoka Wizara ya Ardhi Bw. Mathayo Mitole ameeleza kuwa wananchi ambao wametwaliwa maeneo hawapewi ruhusa ya kuyaendeleza maeneo hayo mara baada ya kufanyiwa uthamini.

“Mtu atakaeendeleza eneo baada ya kufanyiwa uthamini hawezi kuongezewa gharama hivyo kama ni nyumba, kiwanja au shamba vinalipwa kulingana na thamani ya siku ya mwisho ya zoezi la uthamini kumalizika” alisema Bw. Mitole.

Mwananchi kutoka kijiji cha Lusilile wilayani Manyoni Bw. Wiston Said ametoa shukurani kwa serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuleta maendeleo ya nchi hasa vijijini na kuwapatia wananchi waliotwaliwa maeneo yao stahiki zao kwa wakati.

“Miradi mikubwa kama hii ikipita vijijini wanakijiji wanakua na uwanda mpana wa kufanya maendeleo ya kibiashara na kilimo” alisema Bw. Said.

TRC imekua na msaada kwa wananchi waliotwaliwa maeneo kwa kutoa elimu ya uelewa kabla ya wananchi kufidiwa ili kuwapa mwanga wa kujua nini cha kufanya pindi wapatapo malipo yao kwaajili ya kupata maendeleo yao binafsi na taifa.