Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WAENDELEA KUNUFAIKA NA SGR


news title here
18
April
2023

Shirika la Reli Tanzania limeendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa kwaajili ya ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha tano kutoka Isaka hadi Mwanza Aprili 17, 2023.

Ulipaji fidia unafanyika kwa wananchi ambao Ardhi zao zilitwaliwa kwaajili ya kupisha ujenzi wa miundombinu ya njia ya mradi (access road), maeneo ya kumwaga vifusi vinavotokana na ujenzi (damping site) na sehemu za kuchukulia malighafi za ujenzi kama kokoto na mchanga (borrow pits).

Aidha,katika zoezi hilo endelevu la ulipaji fidia takribani wananchi 436 kutoka kijiji cha Iboja Wilaya ya Nzega mkoa wa Tabora na vijiji vya Isaka, Nyanchimbi na Bandari za Wilaya ya Msalala Mkoa wa Shinyanga wanaendelea kulipwa fidia.

Mhandisi wa kipande cha Tano Isaka - Mwanza kutoka Shirika la Reli Tanzania Mhandisi Fanuel Tweve ameeleza kuwa ujenzi wa SGR kipande cha tano hadi sasa kimefikia asilimia 31.6 ya ujenzi ambapo maeneo yanayotumika kuchukulia malighafi (borrow pit) ni 45 sawa na asilimia 98 kulingana na mahitaji ya Mkandarasi na maeneo ya kumwaga vifusi (dump site) ni 19 sawa na asilimia 73 kulingana na mahitaji ya Mkandarasi.

Aidha, Mhandisi Tweve ameongeza kuwa wananchi wa maeneo yanayopitiwa na mradi wamekuwa na hamasa kubwa juu ya ujenzi wa mradi wa SGR hivyo wamekuwa wakitoa Ushirikiano kwa wakandarasi na wataalamu kupitia mazoezi mbalimbali yanayoendelea likiweno la ulipaji fidia.

"Wananchi wa maeneo yanayopitiwa na mradi wamepewa elimu ya kutosha kuhusu ujenzi wa SGR, hii imejenga hamasa na wamekuwa wakitoa ushirikiano vizuri kama unavyoona watu wote hawa maeneo yao yamechukuliwa lakini hakuna aliyelalamika, hii ni dhahiri wanafurahia ujenzi wa SGR" Amesema Mhandisi Tweve.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Iboja Bwana Mabula Masanja ameipongeza Serikali kupitia TRC kwa ujenzi wa mradi mkubwa wa kimkakati kwani licha ya kuwa utaleta maendeleo ya pamoja kwa nchi lakini pia kupitia ujenzi wa SGR maisha ya wananchi yamebadilishwa kupitia ajira mbalimbali na ulipaji fidia wa Ardhi inayotumika katika ujenzi huo.

"Wananchi wa Iboja kwa kweli wamefurahishwa na SGR, naipongeza serikali kwa hatua ya ujenzi wa SGR, kijiji hiki kina nyumba nzuri za kisasa kwasababu ya hizi fidia, naendelea kuwasihi wananchi wangu pesa wanazopata wazitumie kwa malengo mazuri ya familia" Amesema Bwana Mabula.

Bwana Amos Masanja mkazi wa Iboja amelishukuru Shirika la Reli Tanzania kuweza kufanikisha zoezi la ulipaji fidia kwa wakati kwani inajenga uaminifu baina ya wananchi na serikali hivyo kufanikisha ujenzi wa reli ya SGR kwa haraka.

"Mimi nimefurahi sana leo kupokea hundi yangu, mwanzo walivokuja wataalamu wakatuambia tutalipwa niliona ni uongo, lakini leo nimepata pesa yangu nimeanza kuiamini Serikali yangu, kumbe inafanya kweli" Alisema Bwana Amos.