Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WAENDELEA KULIPWA FIDIA KUPISHA UJENZI WA SGR TABORA


news title here
28
May
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC limeendelea na zoezi la uhamasishaji na ulipaji fidia kwa Wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa kwaajili ya kupisha ujenzi wa mradi wa kimkakati wa reli ya kisasa kipande cha nne Tabora - Isaka Mei, 2023.

Katika zoezi hilo la uhamasishaji na ulipaji fidia takribani wananchi 185 kutoka katika vijiji vya Lohumbo, Mwino, Izugawima, Nzubuka na Mogwa Wilaya ya Nzega mkoa wa Tabora wanafidiwa baada ya ardhi zao kutwaliwa kwaajili ya kupisha ujenzi wa njia Kuu ya Reli (Right of Way) na sehemu ya kuchukulia malighafi za ujenzi (Borrow Pits) katika kipande hicho cha nne.

Afisa Ardhi kutoka Shirika la Reli Tanzania Bwana Baraza Valentine amefafanua kuwa kilomita 12.6 ndio sehemu iliyotwaliwa katika vijiji hivyo kwaajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo ya reli ya SGR ikiwemo ujenzi wa njia Kuu ya (Right of way) na sehemu ya kuchukulia vifusi (Borrow Pits) ambapo katika kijiji cha Mogwa kutajengwa sehemu ya kuchukulia vifusi na vijiji vilivyosalia kutajengwa njia kuu ya reli.

"Wananchi hawa wametupa ushirikiano mkubwa wakati wa zoezi la uthamini ,na sasa wanalipwa fidia kwasababu maeneo yao yametwaliwa ili kujenga njia kuu ya reli pamoja na sehemu ya kuchukulia vifusi, zoezi la ulipaji linaendelea vizuri na tunawafidia watu 185 katika vijiji vinne" Alisema Bwana Baraza.

Naye Mzee Sahani Katuli kutoka kijiji cha Lohumbo alieleza furaha yake

"Ninashukuru sana Serikali na Shirika la Reli Tanzania kwa ujenzi huu wa reli ya kisasa-SGR,nina miaka tisini na tatu (93) lakini namuomba Mungu aniwezeshe siku moja nipande treni ya umeme, nimelipwa pesa ya fidia leo shamba langu lilipitiwa na mradi, pesa hii naenda kubadilisha nyumba yangu na kuweka bati jipya".

Naye Bi. Pili Masoud mkazi wa kijiji cha Mwino ambaye ni mfanyabiashara wa mkaa amesema kuwa reli ya SGR itakuwa nyenzo kubwa katika kukuza biashara ndogondogo pindi utakapokamilika na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kiasi kikubwa .

"Ninaamini SGR inaenda kuwa mkombozi wa wafanyabiashara kama mimi, mimi nauza mkaa nategemea SGR ikikamilika nitaweza kuuza mkaa wangu kwenye maeneo yenye masoko makubwa kama Mwanza, Dodoma au Dar Es Salaam ambako kuna walaji wengi na bei kubwa ya kuuza kutokana na mzunguko wa fedha, kwakweli natamani huu mradi ukamilike mapema". Amesema Bi. Pili Masoud.

Ikumbukwe ujenzi wa mradi wa kimkakati wa SGR kipande cha nne kinaendelea ambapo mpaka sasa kipo asilimia 2.3 ya ujenzi.