Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WAAHIDI KUHESHIMU MIPAKA ILIYOWEKWA KWENYE NJIA ZA UMEME MRADI WA SGR


news title here
13
November
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la utwaaji ardhi kupisha mradi wa ujenzi wa reli yenye kiwango cha kimataifa - SGR kipande cha pili Morogoro - Makutupora lililofanyika katika wilaya ya Bahi mkoani Dodoma hivi karibuni Novemba 2023.

Zoezi hilo ni kwaajili ya kupisha njia za umeme pamoja na vivuko ikiwemo vivuko vya njia za juu na za chini vya reli ya SGR ambapo wananchi wameahidi kuheshimu mipaka ya vivuko pamoja na njia ambazo zimepita nyaya za umeme kwaajili ya mradi wa SGR.

Mhandisi mradi kutoka TRC Bw. Ibrahim Kahuru alisema kuwa zoezi la utwaaji ardhi linaambatana na uhamishaji makaburi katika vijiji vya Mzogole, Mpinga, Bahi Makulu na Nagulo ili kupisha vivuko na njia za umeme.

“Zoezi linaenda vyema kwa kushirikiana na uongozi wa vijiji na watu wa afya ambao wanasimamia na kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa kwa kufuata taratibu za kiafya” alisema Mhandisi Ibrahim.

Naye Afisa Afya kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Bi. Restituta Gama alieleza kuwa zoezi linafanyika kitaalamu ili kuzuia maambukizi na milipuko ya magonjwa kwa njia yeyote.

“Tunamwagia dawa kali ambazo zinaua vijidudu kwa haraka sana pia tunahakikisha vitu vyote vya kujikinga kama barakoa, vikinga mikono, ovaroli na mambuti ili mtu asiweze jichoma na mifupa vinakuwepo” alisema Bi. Restituta.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mapinduzi katika kijiji cha Mpinga Bw. Kennedy Gonda ameeleza kuwa wananchi wapo tayari kutosogelea wala kufanya shughuli zozote karibu na mipaka iliyowekwa kwenye nguzo za umeme zilizowekwa na shirika la umeme TANESCO pamoja na njia za vivuko.

Wananchi wanaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika zoezi la utwaaji ardhi kupisha ujenzi wa SGR.