Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WA SHINYANGA WALIPWA FIDIA KUPISHA UJENZI WA RELI YA KISASA KIPANDE CHA ISAKA HADI MWANZA


news title here
19
July
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea kulipa fidia kwa wananchi waliyofanyiwa uthamini wa ardhi na mali zao kupisha ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa - SGR kutoka Isaka hadi Mwanza, Julai 2022.

Zoezi hilo la ulipaji fidia linafanyika chini ya usimamizi wa maafisa wa TRC, viongozi wa serikali za mitaa na vijiji, kwa pamoja maafisa wa TRC na viongozi hao wametoa ufafanuzi kwa wananchi kuwa malipo wanayolipwa yamezingatia Kanuni taratibu na Sheria ya ardhi.

Aidha, viongozi wamewajulisha wananchi kuwa malipo wanayolipwa ni kwaajili ya fidia ya ardhi, mazao, na majengo. Kuhusu wananchi ambao maeneo yao yana makaburi watajulishwa utaratibu wa kulipwa kifuta machozi.

Awamu hii wananchi wa mitaa na vijiji waliolipwa fidia ni 474 katika maeneo ya Gulumuwashi, Iseke ididi, Sumbigu, Bunonga, Negezi, Lubaga, Mwaaza, Mwalugoye, Mwamalili na Azimio.

Afisa jamii kutoka TRC Bi. Joyce Ponera amewaeleza wananchi faida watakazozipata wakati wa ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa kutoka Isaka hadi Mwanza na baada ya ujenzi wa reli hiyo. Bi. Joyce pia amewaasa wananchi watumie fedha hizo za fidia kujipatia maeneo mengine na kujiendeleza kiuchumi .

Kwa upande wa wananchi wameshukuru viongozi wa TRC kwa kutimiza ahadi ya kuwalipa kwa wakati na kuahidi kutumia kwa usahihi fedha wanazolipwa.