Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WA MANISPAA TABORA NA IGALULA WILAYANI UYUI WANUFAIKA NA FIDIA KUTOKA TRC


news title here
01
July
2024

Shirika la Reli Tanzania - TRC limefanya malipo ya fidia Tabora Manispaa na Igalula wilaya ya Uyui mkoani Tabora kwa wananchi waliofanyiwa uthamini wa ardhi kwa ajili ya kupisha ujenzi wa njia kuu ya reli (Right of Way) na stesheni ya SGR Tabora katika kipande cha tatu cha ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR Makutupora - Tabora, Juni 2024.

Mhasibu kutoka TRC Hamad Hamad amesema takribani wananchi 383 wamelipwa fidia katika kitongoji cha Milembela, Timkeni kata ya Uyui - Tabora Manispaa na Igalula pia wengine wanaendelea kulipwa katika ofisi za kata.

"Malipo ya awamu hii yatafanyika pia katika vijiji vya Tambuka reli kata ya Nsololo,Kimungi kata ya Nsololo, Tura na Malongwe kata ya Kizengi wilayani Uyui mkoani Tabora, Shirika linahakikisha kila mwananchi aliyepisha ardhi kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa mradi anapata malipo kwa wakati" ameongeza Hamad.

Afisa Miliki wa TRC Misango Mjandwa amesema wananchi ambao tayari wamelipwa stahiki zao kutokana na uthamini wa ardhi waliofanyiwa wanatakiwa kupisha ardhi zao kwa mujibu wa Sheria ili kumuwezesha mkandarasi kuendelea na shughuli za ujenzi wa mradi katika kipande cha tatu Makutupora - Tabora.

"Wananchi ambao hawajalipwa fidia zao tunaomba wawe watulivu wakati Shirika linakamilisha taratibu za malipo hayo kwa mujibu wa Sheria" amesisitiza Misango.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Milembela kata ya Uyui amepongeza zoezi la malipo kwa wananchi kwani zitawezesha ujenzi wa nyumba na ununuzi wa mashamba kwaajili ya kuendeleza shughuli za kilimo kama ilivyokua awali kabla ya uthamini kufanyika.

Shirika la Reli linaendelea na usimamizi wa ujenzi wa mradi wa kimkakati wa reli ya kiwango cha kimataifa na limeanza uendeshaji wa treni ya abiria katika kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro Juni 14, 2024, Shirika pia linatarajia kuanza uendeshaji wa treni za abiria katika kipande cha pili Morogoro - Makutupora tarehe 25 Julai 2024.