Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI WA FIDIWA KUPISHA UJENZI WA SGR WILAYA YA NZEGA MKOA WA TABORA


news title here
14
May
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC limeendelea na zoezi la uhamasishaji jamii na ulipaji fidia kwa Wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa ili kupisha ujenzi wa mradi wa kimkakati wa reli ya kisasa - SGR kipande cha nne Tabora - Isaka Mei, 2023.

Wananchi takribani 200 katika kata ya Mogwa kijiji cha Mogwa na Ilole Wilaya ya Nzega mkoa wa TABORA wamelipwa fidia baada ya maeneo yao kutwaliwa ili kupisha ujenzi wa reli.

Akifafanua wakati wa zoezi hilo msanifu msimamizi wa mradi kipande cha nne Mhandisi Bright Kahindi ameeleza kuwa wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa ni kwaajili ya kupisha ujenzi wa njia kuu ya reli ya SGR (Right of way) ambapo katika kijiji cha Mogwa kipande kitakachotumika kwenye ujenzi wa njia ni kilomita 4.7 na kijiji cha Ilole kipande kitakachotumika ni kilomita 11.76.

"Wananchi wanaolipwa fidia leo maeneo yao yalichukuliwa ili kujenga njia kuu ya reli (right of way), katika kijiji cha Mogwa tulipima kuanzia kilomita 905 na mita 300 mpaka kilomita 910 sawa na kilomita 4.7 ya kipande ambacho kitajengwa njia ya reli na kijiji cha Ilole kilipimwa kutoka kilomita 898 na mita 200 mpaka kilomita 905 na mita 280 sawa na jumla ya kilomita 11.76 kipande ambacho njia itajengwa" Amesema Mhandisi Bright Kahindi .

Aidha, Mhandisi Kahindi ameongeza kuwa baadhi ya maeneo mengine ambayo yametwaliwa kwa wananchi yatatumika katika ujenzi wa kempu za Mkandarasi, Maeneo ya kutupa vifusi (borrow pits) na Maeneo ya kuchukulia malighafi za ujenzi.

Naye Afisa Mtendaji Kata ya Mogwa ndugu Fabiano Mahenye ameeleza kuwa ujenzi wa SGR na fidia zinazoendelea kulipwa kwa wananchi kutokana na maeneo kutwaliwa na kutumika kwenye ujenzi huo imeleta maendeleo makubwa sana ya kiuchumi na ustawi wa jamii katika vijiji husika.

"Ujenzi wa SGR kwa kweli tumefurahia sana, watu wengi wamehamasika na ujenzi wa reli hii, Leo hapa kwenye fidia hakuna mtu atakaa nyumbani kila mtu anakuja kulipwa stahiki zake na pesa hizi ndo wanajengea nyumba za kisasa kama inavyoonekana tofauti na zamani kulikuwa na nyumba za kiasili" Amesema Bwana Fabiano.

Ujenzi wa SGR unaendelea katika vipande vyote vitano ambapo kipande cha Dar Es Salaam - Morogoro kimefikia asilimia 98.14 ya Ujenzi, Morogoro - Makutupora asilimia 93.83, Makutupora -Tabora asilimia 7, Tabora - Isaka asilimia 2.3 na Mwanza -Isaka asilimia 31.07 za ujenzi.