WANANCHI WA DODOMA WASISITIZWA KULINDA MIUNDOMBINU YA SGR

December
2022
Shirika la Reli Tanzania - TRC likiendelea na kampeni ya uelewa kwa jamii kuhusu usalama na ulinzi wa miundombinu ya reli ya kisasa – SGR limekutana na jamii ya wafugaji na wakulima Dodoma vijijini kutoa elimu elekezi kuhusu matumizi sahihi ya vivuko vya mifugo na matumizi sahihi ya ardhi ili kuepusha uharibifu wa miundombinu ya reli ya kisasa Disemba, 2022.
Maafisa kutoka TRC kwa kushirikiana na wahandisi walifika katika vijiji vya Makutupora, Bahi, Kikombo, Mnase na Chilolo na kufanya mazungumzo wa viongozi wa Serikali ya kijiji na mitaa na kubaini kuwa changamoto ambazo zinawakabili jamii ya wafugaji ni matumizi sahihi ya vivuko kwaajili ya mifugo.
Mara baada ya kubaini adha ya vivuko iliwalazimu kuandaa mkutano wa hadhara na wananchi wakiwemo wafugaji kwaajili ya kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya vivuko vya mifugo na binadamu ili kuepusha madhara yatokanayo na uharibifu na uhujumu wa miundombinu ya reli ya kisasa.
Mhandisi Fredrick Kitaly kutoka kitengo cha ulinzi na usalama wa reli aliwataka wananchi wakiwemo na wafugaji kuacha kuvunja Sheria, kuacha kukata uzio na kufuata vivuko vilivyowekwa ambavyo ni maeneo sahihi ya kuvusha mifugo na maeneo ambayo yametengwa kwaajili ya watu kuvuka.
“Ndugu wananchi na wale wenye mifugo kama nilivyoeleza madhara makubwa ambayo yatajitokeza msipofuata utaratibu wa kuvuka na kuvusha mifugo. Ninawaomba muache kukata uzio uliowekwa na mtumie vivuko vilivyo tayari au vile vya muda. Msivushe mifugo juu ya tuta la reli tumewajengea vivuko na tumeweka alama kama muongozo wa kuwaonesha wapi ni sehemu sahihi ya kuvuka” alisema Mhandisi Kitaly.
Akizungumuza wakati wa mkutano Afisa jamii TRC Bi. Catherine Mwakagali aliwasisitiza wananchi kujenga mazoea ya kupita sehemu sahihi zilizowekwa kwa lengo kulinda miundombinu ya reli na wananchi kubaki salama.
“Mnapoacha kufuata sehemu sahihi za kupita mnapelekea uharibifu wa miundombinu ya reli ikiwemo kuharibika kwa tuta, kutawanyika kwa kokoto, nyasi zilizopandwa pembeni mwa tuta la reli kuliwa na mifugo na kusababisha mmomonyoko wa udongo katika tuta la reli” alisema Bi. Catherine.
Wananchi nao walipewa nafasi ya kueleza changamoto mbalimbali wanazopata wakati wa utekelezaji wa mradi wa SGR. Wananchi wengi hasa wafugaji walibainisha kuwa changamoto kubwa ni umbali pamoja na uchache wa vivuko hivyo kuwalazimu kuvuka na kuvusha mifugo juu ya reli.
Nao Maafisa kutoka TRC waliwasihi wananchi sambamba na wafugaji kueleza changamoto zao zote kwa viongozi wa vijiji na kuzipeleka kwa viongozi wa Shirika la reli ili waweze kutatua na kutoa suluhisho la changamoto ya vivuko na kuwataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kwa kufuata Sheria kipindi ambacho changamoto zinatafutiwa suluhisho.