Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI MKOANI TABORA WAENDELEA KUTOA USHIRIKIANO KATIKA UTWAAJI ARDHI


news title here
16
May
2023

Wananchi waliotwaliwa maeneo yao kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa – SGR kipande cha Makutupora – Tabora waendelea kutoa ushirikiano kwa Shirika la Reli Tanzania – TRC katika zoezi la utwaaji ardhi katika wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Mei 2023.

Shirika la Reli Tanzania linaendelea na zoezi la utwaaji ardhi ili kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha Makutupora – Tabora chenye jumla ya urefu wa kilomita 368, inayojumuisha kilomita 294 za njia kuu na kilomita 74 za njia ya kupishana ambao ujenzi wake umefika asilimia saba (7%).

Shirika limekamilisha uthamini kwa urefu wa kilomita 284 kati ya 294 za njia kuu kwaajili ya kuendelea na taratibu za malipo ili kumkabidhi eneo Mkandarasi kampuni ya Yapi Merkezi kutoka Uturuki kwaajili ya kuendelea na kazi ya ujenzi wa makaravati, tuta, kambi za ujenzi na vituo.

Zoezi la utwaaji ardhi kwa kuhamisha makaburi yaliyopitiwa na mradi linaendelea mkoani Tabora katika vijiji vya Igalula, Goweko, Karangasi na Tura vilivyopo kjatika wilaya ya Uyui ambapo zaidi ya makaburi 700 yanaendelea kuhamishwa ili kupisha mradi wa SGR.

Uhamishaji wa makaburi unafanyika kwa kufuata taratibu za kiafya na zoezi linasimamiwa na ofisi ya Mganga wa Wilaya husika ili kuhakikisha hakuna madhara ya kiafya kwa wananchi wakati wa zoezi la kuhamisha makaburi.

Kabla ya kuanza zoezi la kuhamisha makaburi wananchi katika vijiji vyote walipatiwa elimu ya uelewa kuhusu zoezi la uhamishaji makaburi katika mikutano iliyofanyika katika vijiji kwa nyakati tofauti ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Uyui Bwana Zakaria Mwansasu.

Mwananchi kutoka kijiji cha Igalula mkoani Tabora Bwana Mtuga Saidi ameeleza kuwa amefurahishwa na ushirikiano uliooneshwa na wataalamu kutoka TRC, Maafisa afya Wilaya ya Uyui, Viongozi na wananchi wa kijiji cha Igalula katika zoezi la kuhamisha makaburi ya wapendwa wao kwakuwa taratibu zote zimefuatwa katika zoezi hilo.

Zoezi la utwaaji ardhi hufuatiwa na ulipaji wa fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yamepitiwa na mradi kwa kuzingatia thamani ya ardhi na mali zisizohamishika katika eneo husika. Aidha, Mkandarasi anaweza kukabidhiwa maeneo yaliyo wazi kwa ridhaa ya mmiliki ili aweze kuendelea na kazi huku mwananchi akisubiri malipo ya fidia. Hatua zote hufuata Sheria na taratibu za utwaaji adhri bila kuathiri mmiliki wa eneo lililotwaliwa.