Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WANANCHI MKOANI SHINYANGA NA MWANZA WAPOKEA HUNDI ZA MALIPO YA FIDIA


news title here
15
September
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC limeendelea na zoezi la kukabidhi hundi za malipo ya fidia kwa wananchi waliotwaliwa maeneo yao mkoani Shinyanga na Mwanza, Septemba 2022.

Hundi za malipo ya fidia zaidi ya 200 zimekabidhiwa kwa wananchi mkoani Shinyanga na Mwanza katika vijiji vya Isabilo, Mhulya, Mantare, Ligembe, Bujingu, Sokoni, Ihapa, Mwamalili, Nkalalo, Kang’anga, Ishingisha, Isunga, ili kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha Mwanza - Isaka.

Maeneo yaliyotwaliwa ni pamoja na, maeneo ya njia kuu kwaajili ya kupitisha njia ya reli na maeneo ya kuchukulia udongo unaotumika katika ujenzi wa reli ya kisasa.

Wananchi wa vijiji hivyo wameishukuru Serikali kwa kuwapatia malipo ya fidia ili waweze kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo kilimo, ufugaji pamoja uendelezaji wa makazi kwa kujenga nyumba bora za kuishi.

Mwananchi wa kijiji cha Ihapa mkoani Shinyanga Bwana John Bundara Ndaka amesema kuwa zoezi la malipo ya fidia limekwenda vizuri na ameishukuru Serikali kwa kuwapatia stahiki zao ili waweze kuendelea na shuhuli za kimaendeleo kwani kiasi cha fedha walichopata kupitia fidia hizo kitawawezesha kujenga nyumba za kisasa na kununua ng’ombr na mashamba.

Zoezi limeendeshwa kwa usimamizi wa maafisa kutoka Shirika la Reli Tanzania, maafisa ardhi kutoka wilaya husika, viongozi wa vitongoji na vijiji kwa kushirikiana na maafisa wa benki ili kuhakikisha wananchi wanapata urahisi wa huduma za kibenki ikiwemo kufungua akaunti na kukabidhi hundi kwa usalama zaidi.