Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANANCHI MKOANI DODOMA WAPATA ELIMU KUHUSU KUANZA KWA MRADI WA DARAJA LA GODEGODE


news title here
21
October
2023

Shirika la Reli Tanzania limefanya kampeni ya uelewa kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka mradi wa ujenzi wa daraja la Godegode katika vijiji vya Godegode, Kimagai, Kisisi na Mgoma wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Oktoba 2023.

Lengo la kampeni ni kuwapatia uelewa na utayari wananchi kuhusu mradi wa ujenzi wa daraja na kuinua tuta la reli eneo la Godegode kutokana na changamoto ya uharibifu wa miundombinu unaosababishwa na mafuriko kipindi cha masika. Wananchi wameelezwa kuhusu fursa zitokanazo na mradi ikiwemo fursa za ajira, biashara pamoja na kupata uzoefu, pia wananchi wamefahamishwa masuala mbalimbali kuhusu usalama wa miundombinu ya reli na mambo ya kijamii yanayoambatana na mradi.

Meneja Mradi Msaidizi wa daraja la Godegode Mhandisi Enock Mayala ameeleza kuwa kupitia mradi wa daraja la Godegode “tunatarajia kuinua tuta na kujenga madaraja ili kupitisha maji na kuruhusu shughuli za uendeshaji wa huduma za treni kufanyika kwa kipindi chote cha mwaka, mradi unatarajiwa kufanyika kwa muda wa mwaka mmoja chini ya Mkandarasi kutoka China kampuni ya ‘China Civil Construction Corporation’ (CCECC)”.

Mhandisi Mayala ameongeza kuwa Mkandarasi yuko karibu kuanza mradi lakini kabla ya kuanza mradi upo utaratibu wa kuwashirikisha wadau na kuwapa elimu ya uelewa wa mradi na kuwafahamisha wadau kuhusu changamoto na fursa za mradi ikiwemo Shule ya Msingi Kimagai, Godegode, Shule ya Sekondari Godegode pamoja na wananchi wa vijiji vya Godegode, Kimagai, Kisisi na Mgoma ili kuwashirikisha katika ulinzi na utekelezaji wa mradi.

Wananchi wameupokea vizuri mradi wa ujenzi wa daraja la Godegode utakaoanza rasmi hivi karibuni, mradi utasaidia kutoa suluhisho la kudumu la changamoto ya usafiri wakati wa masika na kuleta maendeleo katika vijiji vinavyozunguka mradi na nchi kwa ujumla.

“kwa kweli mradi huu tumeupokea vizuri kwasababu adha iliyokuwepo hapa ni kwamba kipindi cha masika hakupitiki na sisi tunategemea zaidi usafiri wa reli kwenda stesheni ya jirani Gulwe kwaajili ya kwenda wilayani Mpwapwa, kwahiyo kwa ujio wa mradi huu wa ujenzi wa njia na kujenga daraja tunaupokea vizuri sana” alisema Mwenyekiti wa kijiji cha Godegode Bwana Waziri Ramadhani

Bwana Waziri ameongeza kuwa elimu ya uelewa iliyotolewa kabla ya kuanza kwa mradi ni muhimu na itawasaidia wananchi kutambua mambo mbalimbali yanayoambatana na mradi na namna ya kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi

“kikubwa kilichozungumzwa ni ulinzi wa mali katika mradi pamoja na masuala ya ukatili wa kijinsia yanayoweza kujitokeza katika mradi, elimu hii imetufikia” aliongeza Bwana Waziri

Pamoja na mambo mengine mradi wa Godegode unatarajiwa kuleta fursa za ajira na biashara kwa wananchi wanaozunguka mradi ili kukuza uchumi wa nchi.

“Nitajitahidi kuhakikisha wananchi wanapata fursa za ajira na biashara kwa kuwapa elimu lakini pia itatusaidia kuwepo kwa usafiri wa uhakika kwaajili ya kusafirisha mazao yetu” alisema Mwenyekiti wa kijiji cha Mgoma Bwana Mengi Meshaki