WANANCHI AMBAO HAWAKUWEPO KATIKA UTHAMINI WA AWALI WANAENDELEA KULIPWA FIDIA

June
2022
Zoezi la malipo ya fidia kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR limefanyika kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro na Dodoma ambao hawakuwepo katika uthamini wa awali ili kupisha ujenzi wa vituo vya umeme wa SGR, kipande cha pili (2) Morogoro – Makutupora hivi karibuni Mei, 2022.
Timu ya maafisa kutoka TRC ilianza kwa kutoa taarifa kwa viongozi wa Serikali ya vijiji na kata kwa lengo la kuwatafuta na kuwapa taarifa wananchi ambao hawakuwepo katika uthamini wa awali wa mwaka 2019. Aidha, maafisa wa TRC kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji walifanya jitihada zote za kuwatafuta wamiliki wa maeneo hayo ili waweze kulipwa stahiki zao
Zoezi la malipo ya fidia limeanza rasmi Mkoani Dodoma kwa vijiji saba (7) vyenye jumla ya wananchi takribani 30 ambao wamepewa hundi za malipo kwaajili ya vituo vya umeme sambamba na vijiji kumi na tatu (13) katika mkoa wa Morogoro na Dodoma ambapo jumla ya hundi 118 zinaendelea kulipwa kwa wananchi ambao hawakuwepo wakati wa uthamini wa awali.
Hata hivyo, Afisa Uthamini kutoka TRC Bi. Benlulu Lyimo ameeleza kuwa moja ya changamoto kubwa ambayo ilipelekea wananchi kutokuwepo wakati wa uthamini wa awali ni wananchi kutokuwepo katika maeneo yao wakati wa uthamini na wengine kuishi mikoa ya mbali na maeneo yao hivyo kuchelewa kupata taarifa za uthamini kwa wakati.
Katika hatua nyingine, viongozi wa vijiji walitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikano wakutosha ili kuhakikisha walengwa wa malipo ya fidia wanapatikana kwa wakati ili kuhakikisha wanalipwa stahiki zao na mkandarasi kuendelea na ujenzi wa reli ya kisasa.
Aidha, Tangu mwaka 2017, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipoamua kuanza kujenga miundombinu ya reli ya kisasa, Shirika la reli mchini limeendelea na malipo ya fidia pamoja na kifuta machozi kwa kuhakikisha kwamba wananchi ambao ardhi yao imetwaliwa hulipwa fidia ambayo ni stahiki.